20. Dalili juu ya kwamba kuwategemea waja wema ni shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akisema: “Simshirikishi Allaah na chengine chochote, kamwe, lakini kuwaelekea watu wema sio shirki”. Mwambie: “Ukiwa kweli unakubali ya kwamba Allaah ameharamisha shirki na kwamba ni jambo kubwa kuliko zinaa na unakubali ya kwamba Allaah hatoisamehe, ni jambo gani sasa ambalo Allaah kaharamisha na kusema kwamba hatolisamehe?” Kwa hakika hajui. Mwambie: “Vipi utajitakasa nafsi yako na shirki na wewe huijui? Au vipi Allaah atakuharamishia wewe hili na kutaja ya kwamba hatolisamehe, wakati wewe huliulizii na wala hulijui? Wafikiria ya kwamba Allaah atatuharamishia na wala asitubainishie?” Akisema: “Shirki ni kuabudu masanamu, na sisi hatuabudu masanamu” Mwambie: “Na nini maana ya kuabudu masanamu? Unafikiria ya kwamba walikuwa wakiamini kuwa miti ile na mawe yale yanaumba na yanaruzuku na yanaendesha mambo kwa yule anayeviomba? Hili linakadhibishwa na Qur-aan!”

Akisema: “Ni yule mwenye kuuelekea mti, jiwe au pango lililojengwa kwenye kaburi n.k, anakiomba, kukichinjia na kusema: “Kinatukurubisha kwa Allaah na Allaah anatulinda [na madhara] kwa baraka zake na anatupa kwa baraka zake” Mwambie: “Umesema kweli. Na hichi ndio kitendo chenu kwenye makaburi na majengo yaliyo kwenye makaburi na mengineyo.”

Hili amelikubali ya kwamba kitendo chao hichi ni kuabudu masanamu na ndio jambo lililokuwa linatakikana. Mtu anaweza kumwambia pia: “Kuhusu maneno yako, kwamba shirki ni kuabudu (tu) masanamu, je unamaanisha ya kwamba shirki ni hili tu, na kwamba kuwategemea watu wema na kuwaomba hayaingii katika hiyo [shirki]?” Anaraddiwa[1] na yale aliyoyataja Allaah katika Kitabu Chake kuhusu kukufuru kwa yule ambaye kamtegemea Malaika, ´Iysa na watu wema. Lazima akukubalie ya kwamba mwenye kumshirikisha katika ´Ibaadah ya Allaah miongoni kwa watu wema, ndio shirki iliyotajwa katika Qur-aan, na ndilo lililokuwa linatakikana.

Siri ya mambo ni kwamba akisema: “Mimi simshirikishi Allaah”. Mwambie: “Nieleze, ni nini kumshirikisha Allaah?” Akisema: “Ni kuabudu masanamu” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kuabudu masanamu?” Akisema: “Mimi siabudu isipokuwa Allaah pekee” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kumuabudu Allaah pekee?” Akikueleza kama ilivyoeleza Qur-aan, ndio kinachotakikana. Na ikiwa hajui, vipi atadai kitu na yeye hakijui?

Na akikubainishia kinyume na maana yake, mbainishie Aayah zilizo za wazi za maana ya kumshirikisha Allaah na kuabudu masanamu na kwamba ndio yale yale wayafanyayo leo, na kwamba kumuabudu Allaah pekee hali ya kuwa hana mshirika, ndio yale wanayotupinga kwayo na kutupigia kelele, kama walivyokuwa wakipiga kelele ndugu zao pale waliposeama:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (Swaad 38 : 05)

MAELEZO

Maneno, mahojiano na majadiliano aliyotaja Shaykh (Rahimahu Allaah) juu ya waabudu Malaika na waabudu Mitume ni mambo yako wazi sana. Mwanafunzi akiyasoma basi mambo yatakuwa wazi kwake. Wewe mtake yale yanayolazimisha hoja. Kwa mfano akisema kuwa yeye hamshirikishi Allaah basi muulize maana ya kumshirikisha Allaah. Akijibu kwamba kumshirikisha Allaah ni kule kuyaabudu masanamu, muulize ni nini maana ya kuyaabudu masanamu na kama anafikiria kuwa watu wale walikuwa wakiamini kwamba miti, mawe na majengo yale ndio yenye kuumba na yenye kuruzuku? Haya yanakadhibishwa na Qur-aan. Walikuwa wakikubali ya kwamba Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji. Amesema (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah”, basi sema: ”Je, basi kwa nini hamchi?”[1]

Mambo yako wazi. Baada ya hapo unatakiwa kumuwekea wazi ni nini maana ya kuyaabudu masanamu na kwamba ni kule kuyategemea, kuyataka msaada na kuyawekea nadhiri. Hayo ndio wayafanyayo kwenye makaburi ya waja wema ambapo wanawategemea Malaika, majini na wawatekelezee maombi yao. Ukitambua kuwa matendo haya ni ´ibaadah basi ndio kinachotakiwa. Yale wanayofanya katika kuwategemea mawalii, waja wema, majini na Malaika ndio kumshirikisha Allaah na kwamba vilevile inaweza pia kuwaomba, kuwataka msaada na kuomba baraka kutoka kwao. Kwa hali yoyote wewe unatakiwa kushuka naye katika kila kitu. Kila anapoleta madai fulani basi teremka naye na muombe akufasirie. Akisema kuwa yeye hamshirikishi Allaah basi muulize ni nini maana ya kumshirikisha Allaah. Akisema kuwa yeye hayaabudu masanamu muulize ni nini maana ya kuabudu masanamu. Akifasiri kwa njia inayokwenda kinyume na Shari´ah mwambie ni vipi ataweza kudai kitu asichokijua. Iwapo atafasiri kwa njia inayoafikiana na Shari´ah basi hicho ndicho kinachotakiwa na mwambie kuwa hiyo ndio shirki na ndiyo anayofanya. Wanawategemea wafu, mawe, kuyataka uokozi, kuyawekea nadhiri na kuyachinjia, haya ndio wanayofanya washirikina wa Quraysh na wengineo. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowakemea wakashangazwa na wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[2]

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” wanafanya kiburi na wanasema: “Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu? Bali amekuja kwa haki na amewasadikisha Mitume.”[3]

Wao hawajui ukweli wa mambo wanayofanya, wanajahili shirki na ´ibaadah ambayo wameumbwa kwa ajili yake. Matokeo yake wanapolinganiwa katika haki wanapinga kutokana na ujinga na ukaidi wao na kuwafuata kwao kichwa mchunga wale watangu wao waliopotea. Lakini yule ambaye Allaah anamtakia uongofu anatakiwa kutia akilini na abainikiwe kisha baada ya hapo ndio aafikiane na haki. Huyu ni yule ambaye Allaah anamtakia uongofu, kama hali ilivyokuwa kwa Maswahabah Makkah na al-Madiynah. Yule ambaye Allaah anamtakia uongofu ataikubali haki kama mfano wa as-Swiddiyq, ´Umar baada ya muda mrefu, Twalhah bin ´Ubaydillaah, Zubayr bin al-´Awwaam na wengineo katika Muhaajiruun na Answaar ambao walimpokea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye aliwafunza na baadaye wakarudi kuwalingania watu wao. Walikula kiapo cha usikivu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba watahamia kwao na waeneze Da´wah kati yao. Kwa sababu Allaah aliwatakia uongofu walielewa na wakaikubali haki. Hatimaye wakawa walinganizi wa haki baada ya kwamba walikuwa walinganizi wa batili. Hii ndio fadhilah za Allaah anazomtunuku amtakaye. Amesema (Ta´ala):

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

“Sema: “Kwa fadhilah za Allaah na kwa rehema Zake, basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.”[4]

Ee mja wa Allaah! Jigaragaze kwa Mola wako, muombe Yeye siku zote, akuafikishe, akutunuku elimu, akufungue kifua chako ili uweze kuona ukweli wa mambo ulivyo na uyaona mambo yalivyo. Ni lazima vilevile kwako ujitahidi kusuhubiana na watu wema na ujiepushe na waovu. Ukisuhubiana na wema kutakusaidia juu ya haki na watakuzindua juu ya madhaifu yako. Ama ukisuhubiana na waovu watakupofoza kutoiona haki, watakulingania katika batili na kuwafanyia uadui waliotangulia na watuwazima.

[1] 10:31

[2] 38:05

[3] 37:35-37

[4] 10:58

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 68-72
  • Imechapishwa: 19/10/2021