Ni lazima kumwabudu Allaah pekee, jambo ambalo ndilo analoliridhia. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

”Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[1]

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ

”Yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake.”[2]

Anaridhia kupwekeshwa, Uislamu na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya ndio dini na Uislamu. Ukifanya mambo haya basi utaombewa pamoja na wapwekeshaji wengine juu ya kuingia Peponi. Ikitokea ukaingia Motoni kwa sababu ya madhambi yako basi utakuwa miongoni mwa wale wataopata uombezi midhali umekufa juu ya Tawhiyd na Uislamu.

Kwa kifupi ni kwamba akihoji kama wewe unapinga uombezi mjibu kuwa hupingi bali unauamini na kuuthibitisha. Lakini pamoja na hivyo ni lazima kuuomba kutoka kwa yule Mwenye kuumiliki. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hampi nao yeyote isipokuwa kwanza kwa idihini Yake na aridhie matendo ya yule mwenye kuombewa:

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”[3]

Yeye (Subhaanah) hayuko radhi na shirki. Yuko radhi na Tawhiyd pekee. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[4]

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[5]

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri.”[6]

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[7]

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye na akaridhia.”[8]

Uombezi juu ya watu wataokuwa wamekusanyika kiwanjani hautotokea isipokuwa baada ya idhini Yake (Subhaanah). Uombezi juu ya watu wa Peponi pia ni baada ya idhini Yake. Halafu uombezi juu ya watenda madhambi ni baada ya idhini Yake. Kwa hivyo wewe muombe Allaah, mtakasie Yeye ´ibaadah na hivyo pata bishara ya uombezi.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amepewa uombezi kama walivyopewa wengine. Kwa mfano mawalii na Malaika wamepewa uombezi. Hauhusiani na ule uombezi mkubwa wala uombezi juu ya watu wa Peponi. Inahusiana na uombezi juu ya watenda madhambi. Kwa hivyo haifai kusema kwamba utawaomba uombezi Malaika na mawalii. Ukisema hivo utakuwa umetumbukia ndani ya shirki na kuwaabudu waja wema, mambo ambayo tumekwishayaweka wazi hapo kabla kwamba ni shirki. Na endapo utasema kwamba haifai ndio usawa na haki.

[1] 03:19

[2] 03:85

[3] 21:28

[4] 04:48

[5] 31:13

[6] 39:07

[7] 02:255

[8] 53:26

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 62
  • Imechapishwa: 19/10/2021