19 – Mu´aadhah bint ´Abdillaah al-´Adawiy (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Nilimuuliza ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ni kwa nini mwenye hedhi analipa swawm na halipi swalah. Akasema: “Je, wewe ni Haruuriyyah[1]?” Akasema: “Mimi sio Haruuriyyah. Nauliza tu.” Ndipo akasema: “Tulikuwa tukipatwa na kitu hicho wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunaamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”[2]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha juu ya kwamba mwenye hedhi – anaingia pia mwanamke aliye na damu ya uzazi – haifai kwa wawili hao kufunga. Hili ni kwa maafikiano. Aidha wanatakiwa kula katika Ramadhaan na kulipa. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, pale anapopata hedhi si haswali wala hafungi?” Tukajibu: “Ndio.” Akasema: “Hilo ni miongoni mwa upungufu wa dini yake.”[3]

Hilo ni miongoni mwa rehema za Allaah kwa wanawake. Hakika swalah ni kitu kinajirudirudi kila siku. Na hedhi inajirudirudi kila mwezi aghlabu. Kwa hivyo kuna ugumu mwanamke akilazimishwa kulipa swalah. Kuitekeleza baada ya hedhi kumalizika hakuna haja. Aidha manufaa ya kufanya ´ibaadah kwayo hayampiti kwa kuacha kuilipa. Upande wa pili swawm ni ´ibaadah ya mwaka na hakuna uzito wa kuilipa. Bali swawm ina manufaa kwa mwanamke.

وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا

“Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hekima ya yote.”[4][5]

Mwanamke anapopata hedhi au akapata nifasi sehemu ya mchana, basi swawm yake ya siku hiyo inaharibika. Haijalishi kitu hata kama ni kitambo kidogo kabla ya kuzama kwa jua. Katika hali hiyo atalazimika kulipa siku hiyo. Isipokuwa kama ni swawm ya kujitolea. Atalipa kwa aina ya kujitolea. Kwa sababu ulipaji unasimulia utekelezaji. Mwanamke huyu anatakiwa kula kwa siri kwa kuwa ni sababu yenye kujificha. Asijitangaze ili asijisababishie watu kumtuhumu au akawaghurika wajinga ambapo wakafikiri kuwa kula inafaa pasi na udhuru.

Mwanamke akihisi dalili za hedhi, kama vile maumivu, kuhamahama kwa damu, lakini asitokwe na kitu isipokuwa baada ya kuzama kwa jua, basi funga yake ni sahihi. Hukumu imefungamana na kupatikana kwa hedhi, kitu ambacho hakikupatikana.

Mwenye hedhi akisafika katikati ya mchana wa Ramadhaan, basi haitosihi swawm ya siku hiyo. Kwa sababu kumepatikana kitu ambacho kinapingana na funga mwanzoni mwake. Wako wanazuoni waliosema kuwa anatakiwa kujizuia kula na kunywa sehemu ya siku iliyobaki kwa ajili ya kuheshimu wakati licha ya kwamba analazimika kulipa siku hiyo. Wengine wakasema kuwa hakutomlazimu kwa sababu hafaidiki kitu na kujizuia huko na isitoshe kulipa ni lazima kwake. Allaah ndiye mjuzi zaidi. Haya ya pili ndio maoni dhahiri zaidi. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Akitwahirika usiku katika Ramadhaan – hata kama ni kitambo kidogo kabla ya kupambazuka kwa alfajiri – kwa njia ya kwamba damu ikasimama na akaona kusafika, basi atalazimika kufunga kwa sababu ameingia miongoni mwa watu wanaopaswa kufunga. Haijalishi kitu hata kama hakuoga isipokuwa baada ya kuchomoza kwa alfajiri kama tulivyotangulia kusema. Kwa sababu kuoga sio sharti ya swawm.

Mwanamke mwenye damu ya uzazi akitwahirika kabla ya siku arobaini, basi atalazimika kufunga ikiwa ni ndani ya Ramadhaan. Atafanya yale yanayofanya wanawake waliotwahirika. Kwani hakuna muda wa chini kabisa wa damu ya uzazi.

Damu ya ugonjwa inayomtoka mwanamke haimzuii kufunga. Dalili imethibiti juu ya damu ya hedhi na damu ya uzazi. Jengine ni kwamba damu ya uzazi ni yenye kuendelea na damu ya uzazi ina muda maalum. Aidha damu ya ugonjwa haimzuii mwanamke kuswali wala kutufu Ka´bah. Vivyo hivyo kuhusu swawm. Hili ni kwa maafikiano ya wanazuoni. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Ni unasibisho wa kijiji huko ´Iraaq kilicho karibu na Kuufah. Kundi la kwanza la Khawaarij lilitua hapo lililofanya uasi dhidi ya ´Aliy (Radhiay Allaahu ´anh). Ambaye anaonelea maoni ya Khawaarij anaitwa Haruuriy. Miongoni mwa mambo waliyokuwa wakitilia mkazo katika dini na maoni yao maalum ni kwamba mwanamke mwenye hedhi anapaswa kulipa swalah kama anavyolipa swawm.

[2] al-Bukhaariy (321) na Muslim (335).

[3] al-Bukhaariy (304), (1951), Muslim (132), (79,80).

[4] 04:62

[5] Tazama ”I´ilaam-ul-Muwaqqi´iyn” (02/60).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 22/02/2023