19. Maumbile yaliyosalimika na akili sahihi vinafahamisha kuwepo kwa Muumba

Licha ya hayo maumbile yaliyosalimika na akili sahihi vinafahamisha hayo. Wakati mwingine tunawaona waliodhulumiwa hawawalipizi kisasi wale waliowadhlumu na haki zao hazikuchukuliwa kutoka kwao. Kwa hiyo ni lazima kuwepo na Siku ambayo watafanyiwa hesabu ndani yake na kila mtu atalipwa kwa kile alichotanguliza.

Upande wa pili tunawaona waumini, waja wema, walioongozwa na wenye kujitahidi katika njia ya kheri hawakupata yale yaliyopatwa na wale wa mwanzo ambao wameivuka mipaka ya Allaah na wakawadhulumu waja wa Allaah. Ukiongezea juu ya hayo wako na pesa nyingi, majumba marefu, watumishi na mambo ya anasa. Umati mkubwa wa watu wema na wenye kumcha Allaah hawakuyapata chochote katika mambo haya. Ni lazima kuwepo na Qiyaamah na makutano na Mola wao. Baadhi atawapa daraja za juu na ujira mkubwa. Atawatunuku aina mbalimbali za fadhilah. Hayo ni kutokana na malipo ya subira na matendo yao mema. Hivyo watapata thawabu nyingi, daraja za juu, kheri kubwa, fadhilah kubwa, majumba ya kifakhari, masuria na mema mengine ambayo hayahesabiki kutokana na zile kheri walizofanya na yale matendo mema waliyoyatanguliza. Allaah (Subhaanah) atawalipa madhalimu hawa, waliochupa mpaka na wenye kupuuza ambao wamezama ndani ya dunia na wakadanganyika na matamanio yake na wakaendekeza nyuma ya fitina zake yale wanayostahiki katika adhabu na mwisho mbaya. Haya ni kwa sababu ya kughafilika na kumpuuza kwao Allaah, kuchupa mipaka Yake na kuzikabili neema Zake kwa ukafiri, kuwadhulumu waja Wake na kuyapa mgongo matendo Yake mema. Watu hawa Allaah atawalipa kwa mambo wanayostahiki.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 18/05/2022