Vivyo hivyo baba yetu Aadam ambaye Allaah amemuumba kutokana na udongo na kutoka kizazi kingi kutokana naye. Allaah (Subhaanah) amewaumba kutokana na maji dhalilifu, kisha wakageuka kuwa pande la damu lililoning´inia, kisha kwenda kinofu cha nyama, kisha akawa mtu barabara mwenye kusikia, mwenye kuona, mwenye akili, kudiriki na viungo vya mwili. Kisha akaenda hatua kwa hatua mpaka akawa mtu mkubwa. Akawa anaweza kutwaa, kutoa kumpa mwengine, kufikiria, kujifunza na kuzalisha.

Alama hizi tukufu zote zinajulisha juu ya uwezo wa Allaah na zinafahamisha kuhusu ukweli wa Mitume na wakaeleza ya kwamba huko Aakhirah watakusanyika mbele Yake (Subhaanah). Hapo ndipo haki itapewa nguvu na atawalipa watu wa haki malipo mazuri mno; atawaingiza Peponi na kuwalinda na adhabu ya Moto, kuwadhalilisha maadui Wake na kuwadumisha ndani ya Moto milele.

Kila mwenye busara katika ulimwengu huu anamuona ambaye anadhulumu, ambao zinachukuliwa haki zao, wanaoshambuliwa katika mali zao, miili yao na mengineyo. Mwishowe mkandamizaji huyu anakufa kabla ya kurudisha haki za watu na hakuwafanyia uadilifu wale aliowadhulumu. Je, ina maana kwamba haki hizo ndio zimepotea juu ya wale waliodhulumiwa na wanyonge? Hapana sivyo hivyo! Hakika Muumba, Mkuu, Mwenye hekima, Mjuzi wa kila kitu ameweka wakati maalum kwa ajili ya uadilifu. Wakati huo ni siku ya Qiyaamah ambapo atamfanyia uadilifu yule aliyedhulumiwa ambaye hakupewa haki yake kikamilifu ulimwenguni kutoka kwa yule mkandamizaji. Atamlipiza kisasi na kumwadhibu kwa yale anayostahiki. Ulimwengu sio mahali pa malipo. Hapa ni mahali pa mitihani na majaribio, matendo, mara furaha na mara huzuni. Mara nyingine huenda akafanyiwa uadilifu yule aliyedhulumiwa na hivyo akachukua haki yale ulimwenguni. Pengine wakati mwingine jambo lake likacheleweshwa hadi siku ya Qiyaamah kutokana na hekima kubwa. Hivyo Allaah akawalipiza kisasi wakandamizaji hawa. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ

“Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika si venginevyo anawachelewesha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka.”[1]

Katika siku hii ya kutisha Allaah atawafanyia uadilifu wakandamizwaji na atawapa malipo yao na kuwalipiza kisasi wakandamizaji. Wakati mwingine pengine Allaah akaiharakishia dhuluma adhabu hapa duniani, kama alivofanya juu ya nyumati nyingi. Wakati mwingine pengine akachelewesha jambo hilo kwa ajili ya wale waliodhulumiwa na waliodhulumu kisha watu wakapeana haki katika siku hii tukufu; siku ya Qiyaamah ambayo yatakodolewa macho. Yote haya ni haki.

Mwingi wa hekima, Mjuzi wa kila kitu na Muweza wa kila kitu haipotezi haki ya waliodhulumiwa. Kwa ajili hii ndio maana tukaelezwa kwamba kupo kufufuliwa na kukusanywa, malipo na hesabu. Zipo dalili zilizosimama juu ya haya kutoka katika Qur-aan, Sunnah, maafikiano ya Ummah, akili sahihi na maumbile yaliyosalimika. Vyote hivo vimejulisha ya kwamba ni lazima kuwepo malipo na hesabu, kufufuliwa ni haki, Pepo ni haki, Moto ni haki. Yote hayo yametajwa ndani ya Vitabu vilivyoteremshwa kutoka mbinguni na Sunnah ya kinabii na wameafikiana juu yake waislamu.

[1] 14:42

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 18/05/2022