17. Ambaye huipa ardhi uhai baada ya kufa ndiye atakayewafufua wanadamu

Yale waliyokanusha wakomunisti na makafiri wengine ikiwa ni pamoja na kufufuliwa, kukusanywa, Pepo, Moto na mengine katika yanayohusu siku ya Mwisho yote ni batili na yanakwenda kinyume na dalili zenye kukata. Wote hao hoja zao ni batili na upotofu wake uko wazi. Dalili zinazofahamisha juu ya kuwafufua wafu na kusimama kwao mbele ya Mola wa walimwengu ni nyingi na hazihesabiki. Kila kilichoumbwa na Allaah katika ulimwengu huu ni chenye kushuhudia juu ya uwezo Wake (Subhaanah) na ulazima wa kutambua kuabudiwa Kwake Yeye pekee. Allaah huteremsha mvua juu ya ardhi iliokufa na hivyo mimea ikachipuka kutoka ndani yake baada ya kufa kwake na Yeye (Jalla wa ´Alaa) akaotesha yale matunda ayatakayo. Yule ambaye ameotesha mimea hii na akatuneemesha matunda haya ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ambaye ameteremsha mvua hii ambayo ikahuisha ardhi baada ya kufa kwake na ikaotesha mimea na matunda ndiye ambaye atawapa tena uhai wafu na kuwafufua kutoka ndani ya makaburi yao. Kila mmoja atasimama mbele Yake (´Azza wa Jall) ili kufanyiwa hesabu juu ya yale aliyoyatenda na yale yaliyochumwa na mikono yake katika dunia hii.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 18/05/2022