Sharti za uombezi wenye kuthibitishwa:

1 – Allaah ampe idhini mwombezi kuombea. Allaah hampi idhini yeyote kuwaombea makafiri na washirikina.

2 – Allaah amridhie yule anayeombewa. Allaah hayuko radhi kwa washirikina.

Kwa haya yanabatilika yale maombezi ambayo washirikina wanayaomba kutoka kwa waungu wao. Mtu akimuomba uombezi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kufa kwake, hii ndio shirki. Jambo hili ni miongoni mwa asiyoyaweza yeyote isipokuwa Allaah. Isitoshe amemuomba mwingine asiyekuwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawezi kumuombea yeyote isipokuwa siku ya Qiyaamah. Aidha hawezi kuombea isipokuwa baada ya Allaah kumpa idhini baada ya kumsujudia chini ya ´Arshi, kama ilivyo katika Hadiyth:

“… wamjie Muhammad na wamwambie: “Ee Muhammad! Wewe ni Mtume wa Allaah na ndiye Nabii wa mwisho. Allaah amekusamehe madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja huko mbele. Tuombee kwa Mola wako! Hivi huoni yale tuliyomo?” Nitaenda mpaka nifike chini ya ´Arshi niporomoke hali ya kumsujudia Mola Wangu (´Azza wa Jall) kisha Allaah atanifungulia namna ya kumhimidi na kumsifu kwa uzuri, jambo ambalo hakunifungulia hapo kabla. Kisha kutasemwa: “Ee Muhammad! Inua kichwa chako, omba upewe na fanya uombezi utakubaliwa… “[1]

Dalili ya sharti mbili hizo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Na Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao  isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa Amtakaye na kumridhia.”[2]

Ndani ya Aayah hii kuna sharti mbili; idhini ya Allaah kwa mwombezi aombee na ridhaa Yake kwa yule anayeombewa.

[1] al-Bukhaariy (4712) na Muslim (193).

[2] 53:26

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 139-140
  • Imechapishwa: 06/03/2023