Swali: Ni ipi maana ya kuimba Qur-aan (التغني بالقرآن)?

Jibu: Imepokelewa katika Sunnah Swahiyh mahimizo ya kuimba Qur-aan. Maana yake ni kuisoma kwa sauti nzuri. Maana yake sio kuisoma kama nyimbo. Maana yake ni kuifanya sauti nzuri kwa kisomo. Katika hayo ni ile Hadiyth Swahiyh:

“Allaah hakusikiliza chochote kama alivyomsikiliza Mtume mwenye sauti nzuri ya Qur-aan akiisoma kwa sauti ya juu.”[1]

Hadiyth nyingine inasema:

“Si katika sisi yule asiyeimba Qur-aan hali ya kuisoma kwa sauti.”[2]

Maana yake ni kuisoma kwa sauti nzuri kama ilivyotangulia.

Usikilizaji huu unalingana na Allaah na haufanani na sifa za viumbe Wake. Ni kama zilivyo sifa Zake nyenginezo. Kunasemwa kuhusu kusikia Kwake (Subhaanah) mfano wa yanayosemwa juu ya sifa Zake zengine kwa njia inayolingana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hafanani na yeyote katika chochote (Subhaanahu wa Ta´ala), kama alivosema (´Azza wa Jall):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[3]

Kuisoma kwa sauti nzuri (التغني) ni kule kuisoma kwa sauti ya juu pamoja na kuisoma kwa sauti nzuri na kufanya unyenyekevu kwayo mpaka izitikise zile nyoyo. Kwa sababu lengo ni kuzitikika nyoyo kwa Qur-aan hii ili zinyenyekee, zipate utulivu na zifaidike. Miongoni mwa hayo ni kile kisa cha Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) wake:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipompitia na huku akisoma [Qur-aan] ambapo (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) akimsikiliza akasema:

“Hakika huyu amepewa sauti nzuri katika sauti nzuri za Aal Daawuud.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumkemea jambo hilo. Kwa hiyo ikajulisha kwamba kuinoa na kuifanya sauti ya Qur-aan kuwa nzuri ni jambo linalotakikana ili apate unyenyekevu msomaji, msikilizaji  na wafaidike wote.

[1] al-Bukhaariy (6989) na tamko ni lake, na Muslim (1319).

[2] al-Bukhaariy (6973).

[3] 42:11

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 15/04/2022