77 – Surayj bin Yuunus ametuhadithia: Hushaym ametuhadithia: Yuunus ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan: al-Ahnaf bin Qays amenihadithia:

”Tulikuwa tukihudhuria chakula cha ´Umar. Akitulisha mkate na maziwa, mkate, mafuta na siki, chini ya hivo [tupu] nyama iliyokaushwa na chini ya hivo nyama safi.”

78 – Surayj bin Yuunus ametuhadithia: Hushaym ametuhadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid, kutoka kwa Qays, kutoka kwa ´Utbah bin Farqad as-Sulamiy, ambaye amesema:

”Nilifika kwa ´Umar. Alikuwa akichinja ngamia kila siku na akiwapa nyama waislamu na mama wa Waumini.  Yeye na familia yake wakila shingo na mshipa wa shingo. Siku moja akaomba chakula akaletewa. Basi ilikuwa ni mkate mkubwa na vipande vinene vya nyama. Akanambia mimi nile. Nikajaribu kukata na kumeza, lakini sikuweza. Nikatazama ni kitu gani na kuona kipande cheupe. Nadhani ilikuwa kipande cha nundu, hivyo nikakichukua. Ikadhihiri kwamba ni mshipa wa shingo. ´Umar akanitazama na kusema: ”Huelewi mifupa unayokula wewe na marafiki zako.”

79 – Surayj bin Yuunus ametuhadithia: Marwaan bin Yuunus ametuhadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl bin Abiy Khaalid, kutoka kwa Qays, kutoka kwa ´Utbah bin Farqad, aliyesema:

”Nilimletea ´Umar kikapu cha Khabiysw[1]. Nilipokiweka mbele yake, akafunua sehemu yake na akasema: ”Je, waislamu wote wanapata mambo haya?” Nikasema: ”Hapana, ee kiongozi wa waumini. Haya ni mambo wanayokula watawala peke yao.” Akasema: ”Basi sikihitaji.” Kisha akaitaja Hadiyth.

80 – Khaalid bin Mirdaas as-Sarraaj ametuhadithia: ´Abdullaah bin al-Mubaarak ametuhadithia, kutoka kwa ´Ubaydullaah bin al-Waliyd, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Ubayd, ambaye amesimulia kuwa ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

”Enyi Wahajiri! Msikithitishe kuwatembelea watu wanaopenda dunia. Kwani ina athari ya kukasirisha katika riziki.”

81 – Khaalid bin Mirdaas ametuhadithia: al-Mu´allaa al-Ju´fiy ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Najiyh, kutoka kwaa Mujaahid, ambaye ameeleza kuwa ´Umar amesema:

”Enyi watu! Jihadharini kunenepa kutokana na chakula. Kwani kunamfanya mtu kuwa na uvivu kutokana na swalah, kunauharibu mwili na kunasababisha maradhi. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anamchukia mwanachuoni mnene. Kuleni wastani ili kuwa karibu zaidi inavyowezekana na usahihi, kuwa mbali zaidi inavyowezekana kutokana na israfu na kupata nguvu zaidi inavyowezekana katika kumwabudu Allaah. Hakika mja hatoangamia mpaka pale atakapoyatanguliza mbele matamanio yake mbele ya dini yake.”

[1] Tamtam iliyotengenezwa kwa tende na siagi. 

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 70-72
  • Imechapishwa: 20/06/2023