Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hakika msafiri na mgonjwa wanazo hukumu walizoruhusiwa na Mwekaji Shari´ah ikiwa ni pamoja na:

1 – Inafaa kwa msafiri ndani ya mwezi wa Ramadhaan kula kipindi cha safari yake. Baadaye atalipa muda wa zile siku alizokula. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ َ

“Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[1]

2 – Msafiri ambaye amefunga ndani ya mwezi wa Ramadhaan ni mwenye kupewa khiyari kati ya kufunga na kuacha kufunga. Akiwa atakula baadaye atatakiwa kulipa. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kuwa Hamzah bin ´Imraan al-Aslamiy alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, nifunge nikiwa safarini?” – mtu huyu alikuwa ni mwenye kufunga sana – akamjibu: “Ukitaka funga na ukitaka kula.”[2]

Wanazuoni wametofautiana ni kipi bora kufanya? Wako waliosema kuwa kula ndio bora zaidi kwa sababu ya kutendea kazi ruhusa ya Allaah. Wengine wakasema kuwa kufunga ndio bora zaidi kwa sababu ya kutakasa dhimma. Haya ya pili ndio maoni sahihi zaidi. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

3 – Inafaa kwa mgonjwa kula mchana wa Ramadhaan na baadaye atalipa masiku aliyokula. Vivyo hivyo inamuhusu mjamzito na mnyonyeshaji watapochelea juu ya afya zao au juu ya afya za watoto wao. Katika hiyo itafaa wao kula na baadaye watalipa. Kwa sababu wana hukumu moja kama mgonjwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ َ

“Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[3]

Ugonjwa unaomruhusu mtu kutokufunga ni yale maradhi makali ambayo yanaongezeka iwapo atafunga au kunakhofiwa yakachelewa kupona[4].

Wanazuoni wameafikiana kwa jumla juu ya kufaa kula kwa mgonjwa. Hilo ni kutokana na maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini.”[5]

Hilo ni tofauti na maradhi mepesi ambayo hayamtaabishi endapo atafunga wala funga haimwathiri chochote. Katika hali hiyo haitoruhusu kwake kula. Bali atalazimika kufunga kwa sababu anaingia katika jumla ya maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”[6]

Allaah awawafikishe wote kumtii, awaruzuku wote elimu yenye manufaa na matendo mema.

Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121).

[3] 02:185

[4] Tazama ”al-Mughniy” (03/155) ya Ibn Qudaamah.

[5] 22:78

[6] 02:185

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 19/04/2023