17. Makatazo ya kuwaomba viumbe uombezi na kumuomba Allaah pekee

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Akisema: “Je, wewe unapinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuikana?” Mwambie: “Siipingi na wala siikani, bali yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye muombezi wa waombezi na nataraji kupata uombezi wake, lakini maombezi yote ni ya Allaah (Ta´ala). Kama alivyosema (Ta´ala):

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema: “Uombezi wote ni wa Allaah.” (az-Zumar 39 : 44)

Na wala hautofanya kazi isipokuwa baada ya idhini ya Allaah. Kama alivyosema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (al-Baqarah 02 : 255)

Na wala Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatomwombea yeyote isipokuwa baada ya Allaah kumruhusu. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (al-Anbiyaa´ 21 : 28)

Na Yeye (Subhaanah) haridhii jengine isipokuwa Tawhiyd. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ

”Yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake.” (Aal ´Imraan 03 : 85)

Ikiwa uombezi wote ni wa Allaah na wala hautokuwa isipokuwa baada ya idhini Yake, na wala Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala mwengine hawatomwombea yeyote mpaka Allaah amruhusu – na wala Allaah haridhii isipokuwa watu wa Tawhiyd – imekubainikia ya kwamba uombezi wote ni wa Allaah. Hivyo basi, mimi nautafuta kutoka Kwake. Ninasema: “Ee Allaah, usiniharamishie uombezi wake, Ee Allaah, ninakuomba aniombee” na mfano wa haya. Akisema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kapewa uombezi na mimi naomba kile alichompa Allaah.” Jibu ni kuwa: “Ni kweli kuwa Allaah kampa uombezi, lakini amekukataza hili2. Kasema ”Msiombe yeyote pamoja na Allaah.”. Ikiwa utamuomba Allaah akupe uombezi wa Mtume, tii Kauli Yake:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

Isitoshe uombezi wamepewa wengine asiyekuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imesihi ya kwamba Malaika wataombea, mawalii wataombea na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe wataombea. Utasema ya kwamba: “Kwa vile Allaah kawapa uombezi hivyo nitaiomba kutoka kwao?” Ukisema hivyo, utakuwa umerejea katika kuwaabudu watu wema ambao Allaah kawataja katika Kitabu Chake. Na ukisema: “Hapana”, kauli yako inakuwa batili: “Allaah Kawapa uombezi na mimi ninaomba kile alichowapa Allaah.”

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amezungumza kwa upambanuzi kuhusiana na uombezi. Amefanya vizuri katika jambo hilo. Ameweka wazi yale yanayotakiwa kuwekwa wazi na yale ambayo ndani yake kuna hoja yenye kukata kabisa dhidi ya washirikina. Akisema kuwa yeye anaomba uombezi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akauliza kama sisi tunapinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kujitenga nao mbali, basi mjibu kwamba wewe huupingi na wala hujitengi nao mbali. Bali unauthibitisha. Allaah amewapa Mitume, Manabii na Malaika haki ya kuombea na kwamba yote hayo ni haki. Allaah amewapa uombezi na amekukataza wewe kuwaomba wao. Kwa sababu ni miliki ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Ta´ala):

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema: “Uombezi wote ni wa Allaah.”[1]

Ni miliki anayompa amtakaye. Hivyo tunauomba kutoka kwa yule Mwenye kuumiliki. Isitoshe ni kwamba Yeye (Subhaanah) hakuna yeyote anayeomba mbele Yake isipokuwa kwa idhini Yake. Jengine hampi idhini yeyote isipokuwa wapwekeshaji na anaridhia matendo yao pekee. Kwa hivyo kuuomba kutoka kwa mtu – ni mamoja awe Mtume, mtoto mdogo, Malaika au walii – ni kuuomba kutoka kwa ambaye haumiliki. Mwenye kumiliki uombezi ni Allaah:

قُل لِّلَّـهِ الشَّفَاعَةُ جَمِيعًا

”Sema: “Uombezi wote ni wa Allaah.”

Kuomba uombezi kutoka kwa wengine asiyekuwa Allaah ni kutumbukia ndani ya shirki. Kwa sababu kuwaomba, kuwataka msaada na kuwawekea nadhiri ni kuwashirikisha. Isitoshe hili linapingana na maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[2]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[3]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

”Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu”[4]

ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

 “Niombeni Nitakuitikieni.”[5]

Ambalo ni wajibu ni kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) uombezi na kumfanyia du´aa Yeye pekee. Kwa sababu ni miliki Yake na hampi nao isipokuwa yule ambaye ameridhia kutoka Kwake maneno na matendo Yake. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”[6]

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye na akaridhia.”[7]

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri.”[8]

Hayuko radhi waja Wake wakufuru.

[1] 39:44

[2] 72:18

[3] 17:23

[4] 02:21

[5] 40:60

[6] 21:28

[7] 53:26

[8] 39:07

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 60-62
  • Imechapishwa: 18/10/2021