16. Kugawanyika kwa washirikina katika kuiacha haki

Kwa haya zinapata kubainika shubuha za washirikina na kwamba mwenye kuzipambanua, akazindukana nazo na akajadiliana nao kwa hekima na njia nzuri basi mambo yatakuwa wazi kwake kwa yule ambaye Allaah anamtakia uongofu. Ama kuhusu yule ambaye Allaah anamtakia maangamivu hakuna namna kwake. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ

“Lakini ishara zote na maonyo haiwafai kitu watu wasioamini.”[1]

إِنَّ الَّذِينَ حَقَّتْ عَلَيْهِمْ كَلِمَتُ رَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ

”Hakika wale ambao neno la Mola Wako limethibiti juu yao hawataamini. Japokuwa itawajia kila alama mpaka waone adhabu iumizayo.”[2]

Yule ambaye ameshahukumiwa maangamivu haitomnufaisha kitu. Bali atapinga na kukataa:

وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ

“Japokuwa itawajia kila alama.”

Abu Jahl, ´Utbah bin Rabiy´ah na mfano wao walijiwa na alama. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaonyesha alama lakini hata hivyo wakazikanusha kwa sababu ya ukaidi. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[3]

Namna hii ndivo wanavopinga. Amesema kuhusu watu wa Fir´awn:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا

“Wakazipinga kwa dhuluma na majivuno na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha. “[4]

Kinacholengwa ni kwamba maadui wengi wa Allaah wanaipinga haki kwa kukanusha tu na kufanya inda na si kwa sababu eti wana mashaka juu ya yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini kinachowapelekea katika hayo ni ukaidi na kupenda mali kama alivofanya yule msomi ambaye aliachana na dini yake ilihali anajua kuwa Muusa amekuja na haki. Pamoja na hivyo akaachana na haki kwa sababu ya kuwatii watu wake na kuipa kipaumbele dunia mbele ya Aakhirah na hatimaye Allaah akamwangamiza na kumpokonya elimu na imani.

Kinacholengwa ni kwamba washirikina wamegawanyika mafungu mbalimbali. Miongoni mwao wako ambao ni wajinga ambao ujinga umewapindukia. Amesema (Ta´ala):

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا

“Je, unadhania kwamba wengi wao wanasikia au wanatia akilini? Si vyenginevyo isipokuwa ni kama wanyama, bali wao wamepotea zaidi njia.”[5]

Hii ndio hali ya wengi.

Wako wengine ambao wanakufuru kwa sababu ya inda, ukaidi na kiburi. Vinginevyo wanatambua kuwa haki iko pamoja na Mitume na waumini. Lakini hata hivyo wanasema kuwa hawawafuati na hawako radhi kuwafuata waislamu. Yote haya kwa sababu ya kufanya kiburi, ukaidi na dhuluma. Inawezekana vilevile ikawa ni kwa sababu ya mali anayopokea au kazi atayopata. Endapo atajisalimisha basi ataondoshwa. Matokeo yake anaacha kufuata Uislamu kwa sababu ya kazi atayopewa, kwa sababu ya mali anayopokea, mapenzi kuwapenda ndugu na awe pamoja nao kwenye ukafiri wao na mfano wa hayo kama hali ilivyo kwa makafiri wengi wa Quraysh. Dhuluma, hasadi, ukaidi na kiburi viliwafanya kuipinga haki na kutokuwa radhi nayo. Baadhi yao ni Abu Jahl, ´Utbah bin Rabiy´ah, Shaybah bin Rabiy´ah na wengineo. Mwengine ni ami yake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni Abu Twaalib.

[1] 10:101

[2] 10:96-97

[3] 06:33

[4] 27:14

[5] 25:44

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 54-55
  • Imechapishwa: 18/10/2021