15. Radd kwa mwenye kudai kwamba du´aa sio ´Ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Jua ya kwamba shubuha hizi tatu ndio kubwa walizonazo. Pale utapojua kuwa Allaah katuwekea nazo wazi katika Kitabu Chake na ukazifahamu vizuri, yaliyo baada yake yatakuwa sahali zaidi kuliko hayo. Akisema: “Mimi siabudu mwengine yeyote isipokuwa Allaah na huku kutafuta kinga kutoka kwao [watu wema] na kuwaomba [du´aa] sio ´Ibaadah”, mwambie: “Wewe unakubali kuwa Allaah kafaradhisha juu yako kumtakasia ´Ibaadah na ni haki Yake juu yako?” Akisema: “Ndio”. Mwambie: “Nibainishie hili ulilofaradhishiwa juu yako, ambalo ni kumtakasia ´Ibaadah Allaah pekee, jambo ambalo ni haki Yake juu yako!” Ikiwa hajui ´Ibaadah ni kitu gani na wala aina zake, basi mbainishie yale Allaah (Ta´ala) anayosema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye hawapendi wenye kuvuka mipaka.” (al-A´raaf 07 : 55)

Ukishamjulisha hayo, mwambie: “Unajua sasa kuwa hii ni ´Ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio” – na du´aa ndio kichwa cha ´Ibaadah. Mwambie: “Ikiwa umekubaliana na mimi ya kwamba ni ´Ibaadah na ukamuomba Allaah usiku na mchana, kwa khofu na unyenyekevu, kisha ukamuomba haja hiyo Mtume au mwengine; je utakuwa umeshirikisha katika ´Ibaada ya Allaah asiyekuwa Yeye?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Kwa hiyo unajua Kauli ya (Ta´ala):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na [pia ukichinja] na chinja [kwa ajili Yake]!” (al-Kawthar 108 : 02)

ukamtii Allaah na ukamchinjia; je hii itazingatiwa kuwa ni ´Ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Ukimchinjia kiumbe, sawa awe ni Mtume, jini au wengine, je, utakuwa umeshirikisha katika ´Ibaadah hii asiyekuwa Allaah?” Hana budi kukubali na kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Washirikina ambao waliteremshiwa Qur-aan, je walikuwa wakiabudu Malaika, watu wema, Laat na wengineo?” Hana budi kusema: “Ndio”. Hivyo mwambie: “Je, kuwaabudu kwao ilikuwa tu ni katika du´aa, kuchinja na kutafuta kinga kwao na mfano wa hayo? Vinginevyo walikuwa wakikiri kuwa ni waja Wake, chini ya uwezo Wake na kwamba Allaah ndiye Mwenye kuyaendesha mambo, lakini waliwaomba na kuwategemea kwa sababu walikuwa na jaha na maombezi – na hili ni jambo liko wazi sana.”

MAELEZO

Ukishatambua kuwa shubuha hizi tatu kumeshabaini ubatilifu wake – na ndio kubwa walizonazo – ndipo utajua kuwa zilizo baada yake ni nyonge zaidi. Kumeshatangulia shubuha tatu ambapo moja wapo wanasema kuwa washirikina hawashirikishi pamoja na Allaah katika uumbaji na uruzukaji na maneno ya mwenye kusema kwamba yeye hashirikishi pamoja na Allaah chochote. Bali anadai kwamba anaamini kuwa Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji. Mbainishie kwamba washirikina hawakushirikisha katika uumbaji. Walikuwa wakikiri kwamba Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji.

Vivyo hivyo akisema kuwa shirki ni kuyaabudu masanamu, basi mbainishie kuwa shirki ni kuyaabudu masanamu na visivyokuwa masanamu. Akisema kwamba yeye hawaabudu waja wema na kwamba eti anajikurubisha kwao ili wamuombee, basi mweleze kuwa washirikina walikuwa na malengo hayohayo. Hawakuwaabudu kwa sababu wanaumba au wanaruzuku. Waliwaabudu ili wawaombee na wawakurubishe mbele ya Allaah. Mweleze kwamba hayo anayoyafanya ndio yaleyale yaliyofanywa na washirikina wa kale. Kumekwishabainika ubatilifu wa utata huu na kumebaini kuwa washirikina walikuwa wakikubali kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba, Mwenye kuruzuku, ndiye Mola wao na kwamba shirki yao ilikuwa katika mambo mengine kwa kujikurubisha kwa asiyekuwa Allaah kwa kuwafanyia ´ibaadah. Ametambua pia kuwa shirki ya washirikina haikukomeka kuyaabudu masanamu peke yake. Bali miongoni mwao wako walioyaabudu masanamu, Malaika, Mitume na waja wema. Ametambua pia kwamba aliwaabudu ili wawakurubishe mbele ya Allaah ili wawaombee. Malengo ya hawa waliokuja nyuma ndio yaleyale ya wale waliotangulia hapo kale.

Ukishazijua shubuha hizi tatu basi utatambua kuwa zilizo baada yake ndio rahisi zaidi. Ni jambo linalotambulika kuwa wale wa mwanzo walikuwa wanaamini kuwa Allaah ndiye Mwenye kuumba, Mwenye kuruzuku na Mwenye kuyaendesha mambo. Pamoja na haya yote Allaah aliwahukumu ukafiri na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita na akahalalisha damu na mali zao. Vivyo hivyo yanawahusu wale waliokuja baada yao. Pamoja na hivyo akisema kuwa yeye hamwabudu mwengine asiyekuwa Allaah, basi muulize na muombe akufasirie ni nini maana ya kumwabudu Allaah. Akisema kuwa yeye anakiri kuwa Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji mjibu kwa yale yaliyotangulia kwamba hayo waliyakubali pia washirikina. Washirikina walikubali kwamba Allaah ndiye Muumbaji, Mruzukaji na Mwenye kuyaendesha mambo yao. Akisema kuwa yeye hamwabudu mwengine isipokuwa Allaah isipokuwa tu anaamini kuwa waja wema wataombea na wanaweza kusogeza karibu, basi mweleze kuwa huo ndio ushirikina wa wale wa mwanzo. Muombe akufasirie ni nini kumwabudu Allaah na akajibu kuwa ni kule kumuomba, kumuomba akuongoze, akupe riziki na kumuomba uokozi, basi muulize endapo akimtekelezea mambo hayo mwengine asiyekuwa Allaah kama mfano wa walii, sanamu, jini na Malaika, je, atakuwa hakumshirikisha Yeye katika ´ibaadah? Ni lazima akubali. Vilevile muulize mtu akiswali na akichinja kwa ajili ya Allaah, je, atakuwa amefanya ´ibaadah? Ni lazima akubali. Kwa hivyo mweleze iwapo atachinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah, kama mfano akachinja ngamia, ng´ombe au kondoo kwa ajili ya sanamu, akaswali au akasujudu kwa ajili yake, je, atakuwa amefanya ´ibaadah? Ni lazima akubali.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 51-54
  • Imechapishwa: 18/10/2021