17- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiifungua swalah yake kwa du´aa mbalimbali. Akimhimidi Allaah, anamtukuza na kumsifu. Alimwamrisha hayo yule aliyeswali kimakosa na kumwambia:

“Haitimii swalah ya mtu yeyote mpaka alete Takbiyr, amhimidi na kumsifu Allaah (´Azza wa Jall) na kusoma kile kitachomkuwia wepesi katika Qur-aan.”[1]

Mara alikuwa akisoma du´aa hizi na mara nyingine zile. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma:

اللَّهُمَّ بَاعِدْ بَيْنِي وَبَيْنَ خَطَايَايَ كَمَا باعَدْتَ بَيْنَ الْمَشْرِقِ والْمَغْرِبِ اللَّهُمَّ نَقِّنِي مِنْ خَطَايَايَ كَمَا يُنَقَّى الثَّوْبُ الأَبْيَضُ مِن الدَّنَسِ اللَّهُمَّ اغْسِلْنِي مِنْ خَطَايَايَ بالثَّلْجِ والْمَاءِ والْبَرَدِ

“Ee Allaah! Nitenge baina yangu mimi na makosa yangu kama ulivyotenga baina ya mashariki na magharibi. Ee Allaah! Nitakase madhambi yangu kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokamana na uchafu. Ee Allaah! Nisafishe kutokamana na madhambi yangu kwa maji, theluji na baridi.”

Aliisoma katika swalah ya faradhi.[2]

Alisoma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile:

وَجَّهْتُ وَجْهِي للَّذِي فَطرَ السَّمَواتِ والأَرْضَ حَنيفاً وَما أَنا مِنَ الْمُشْرِكِينَ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي للهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أول الْمُسْلِمِينَ اللَّهُمَّ أَنْتَ الْمَلِكُ لاَ إِلهَ إِلاَّ أَنْتَ رَبِّي وَأَنَا عَبْدُكَ ظَلَمْتُ نَفْسِي واعْتَرَفْتُ بِذَنْبِي فَاغْفِرْ لِي ذُنُوبِي جَمِيعاً فإِنَّهُ لاَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ واهْدِنِي لأَحْسَنَ الأَخْلاَقِ لاَ يَهْدِي لأَحْسَنِهَا إِلاَّ أَنْتَ واصْرِفْ عَنِّي سَيِّئَها لاَ يَصْرِفُ عَني سَيِّئَهَا إِلاَّ أَنْتَ لَبَّيْك وَسَعْدَيْكَ والْخَيْرُ كُلُّهُ في يَدَيْكَ وَالشَّرُّ لَيْسَ إِلَيْكَ أَنا بِكَ وإِلَيْكَ تَبَارَكْتَ وَتَعَالَيْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وأَتُوبُ إِلَيْكَ

“Nimeuelekeza uso wangu kikweli kwa Yule aliyeumba mbingu na ardhi, hali ya kumtakasia Yeye dini yangu, nami sikuwa miongoni mwa washirikina. Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah, Mola wa walimwengu, Asiyekuwa na mshirika; hayo ndiyo niliyoamrishwa na mimi ndiye wa kwanza katika waislamu. Ee Allaah! Wewe ni mfalme! Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe. Wewe ndiye Mola wangu na mimi ni mja Wako. Nimeidhulumu nafsi yangu na nimeyakubali madhambi yangu. Hivyo nisamehe madhambi yangu yote. Kwani hakuna mwengine anayesamehe madhambi isipokuwa Wewe. Niongoze katika zile tabia njema. Kwani hakuna mwengine anayeongoza katika tabia njema isipokuwa Wewe. Nikinge na zile mbaya. Kwani hakuna mwengine anayekinga [tabia] mbaya isipokuwa Wewe. Nakuitikia na nafuata amri Yako[3]. Kheri zote zinapatikana mikononi Mwako. Shari haitoki Kwako[4]. Mimi niko kwa ajili Yako na ni wa Kwako. Umetukuka na uko juu. Nakuomba msamaha na kutubia Kwako.”

Alisoma hivo katika swalah ya faradhi na ya sunnah[5]. Hali kadhalika du´aa hii pasi na:

أَنْتَ رَبِّي وَأَنَا عَبْدُكَ

“Wewe ndiye Mola wangu na mimi ni mja Wako”

ambayo badala yake akizidisha:

اللهم أنت الملك لا اله إلا أنت سبحانك و بحمدك

“Ee Allaah! Wewe ndiye Mfalme. Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe. Umetakasika na himdi zote ni Zako.”[6]

4- Akisoma mfano wake mpaka katika:

وَأَنَا أول الْمُسْلِمِينَ

“… na mimi ndiye wa kwanza katika waislamu.”

na akizidisha:

اللهم اهدني لأحسن الأخلاق و أحسن الاعمال, لا يهدني لأحسنها إلا أنت، و قني سيء الأخلاق و الاعمال، لا يقي سيئها إلا أنت

“Ee Allaah! Niongoze katika zile tabia njema na matendo mema. Kwani hakuna mwengine anayeongoza katika tabia njema isipokuwa Wewe. Nikinge na zile mbaya na yale matendo mabaya. Kwani hakuna mwengine anayekinga hayo mabaya isipokuwa Wewe.”[7]

5-

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako[8], ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako[9], ufalme Wako ni mkubwa[10] na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”[11]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika maneno yanayopendwa kabisa na Allaah ni mja kusema:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”[12]

6- Katika swalah ya usiku alisoma du´aa hiyo hiyo na kuongeza:

لا اله إلا الله

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

Alisoma hivo mara tatu. Kisha akasoma:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Alisoma hivo pia mara tatu.

7-

الله أَكْبَرُ كَبِيراً والْحَمْدُ للهِ كَثِيراً وَسُبْحَانَ اللهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً

“Hakika Allaah ni mkubwa. Himdi Zake ni nyingi. Ametakasika Allaah asubuhi na jioni.”

Kuna Swahabah aliifungua swalah yake hivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nimependezwa nayo. Imefunguliwa milango ya mbinguni.”[13]

8- Kuna mwingine aliifungua swalah yake kwa kusema:

الحمد لله حمداً كَثِيراً طَيِّبَاً مُبَاركاً فيه

“Himdi zote zinamstahikia Allaah – himdi nyingi, nzuri na zilizobarikiwa.”

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Nimeona Malaika kumi na mbili wakishindana ni nani ataanza kuipandisha juu.”[14]

9-

اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ أَنْتَ نُورُ السَّمَاواتِ والأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ وَلَكَ الْحَمْدُ أَنْتَ قيّام السَّماواتِ والأَرْضِ وَمَنْ فِيهِنَّ وَلَكَ الْحَمْدُ أَنْتَ رب السماواتِ و الأرضِ و من فيهن أنت الحق وَعْدُكَ الْحَقُّ وَقَوْلُكَ الْحَقُّ وَلِقَاؤُكَ حَقٌّ والْجَنَّةُ حَقٌّ وَالنَّارُ حَقٌّ والنَّبِيُّونَ حَقٌّ وَمُحَمَّدٌ حَقٌّ وَالسَّاعَةُ حَقٌّ اللَّهُمَّ لَكَ أَسْلَمْتُ وَبِكَ آمَنْتُ وَعَلَيْكَ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْكَ أَنَبْتُ وَبِكَ خَاصَمْتُ وَإِلَيْكَ حَاكَمْتُ فاغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ وَمَا أَخَّرْتُ ومَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ و ما أنت أعلم به مني، أنت القدم و أنت المؤخر أَنْتَ إِلهي لاَ إِله إِلاَّ أَنتَ و لا حول و لا قوة إلا بك

“Ee Allaah! Himdi zote ni Zako. Wewe ndiye mwangaza wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Himdi zote ni Zako. Wewe ndiye mwenye kuzisimamia mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Himdi zote ni Zako. Wewe ndiye Mola wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Wewe ni Haki. Ahadi Yako ni haki. Neno Lako ni haki. Kukutana na Wewe ni haki. Pepo ni haki. Moto ni haki. Mitume ni haki. Muhammad ni haki. Qiyaamah ni haki. Ee Allaah! Kwako nimejisalimisha. Wewe nimekuamini. Kwako nimeamini. Kwako nategemea. Kwako ni mwenye kurejea. Nimepigana kwa ajili Yako. Nakuacha uhukumu. Nisamehe yale niliyoyatanguliza na niliyoyachelewesha, niliyoyaficha, niliyoyaonyesha na yale Wewe unayoyajua zaidi kuliko Mimi. Wewe ndiye unayatanguliza mambo pahala stahiki na Wewe ndiye unayachelewesha mambo pahala stahiki. Wewe ndiye Mungu wangu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe. Hapana njia wala uwezo isipokuwa kupitia Kwako.”[15]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiisoma katika swalah ya usiku kama mfano vilevile wa du´aa zifuatazo:

10-

اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَالَ وَإِسْرَافِيلَ فَاطِرَ السَّمَواتِ والأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ والشَّهَادَةِ أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادك فِيما كانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بإِذْنِكَ إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلى صِرَاطٍ مُسْتَقِيم

“Ee Allaah! Mola wa Jibriyl, Mikaa-iyl na Israafiyl. Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa vilivyojificha na vyenye kuonekana! Hakika wewe [siku moja] utahukumu kati ya waja Wako katika yale waliyokuwa wakitofautiana! Niongoze mimi katika haki katika yale waliotafautiana kwa idhini Yako – Hakika Wewe unamuongoza umtakae katika njia ilionyoka.”[16]

11- Alikuwa akizisoma du´aa hizi kila moja mara kumi:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

الحمد لله

“Himdi zote zinamstahikia Allaah.”

سبحان الله

“Allaah ametakasika.”

لا اله إلا الله

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.”

أستغفر الله

“Ninamuomba Allaah msamaha.”

Baada ya hapo anasoma du´aa ifuatayo mara kumi:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لي وَاهدِني وَ ارْزُقْني وَ عَافِنِي

“Ee Allaah! Nisamehe, niongoze, niruzuku na uniafu.”

Halafu akisema maneno yafuatayo mara kumi:

اللهم إني أعوذ بك من الضيق يوم الحساب

“Ee Allaah! Najilinda Kwako na dhiki za siku ya Hesabu.”[17]

12-

الله أكبر الله أكبر الله أكبر ذو الجبروتِ وَالملكوتِ والْكِبْرِياءِ والْعَظَمة

“Allaah ni mkubwa! Allaah ni mkubwa! Allaah ni mkubwa! Aliye na ufalme na uola, nguvu na utukufu.”[18]

[1] Abuu Daawuud na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[2] al-Bukhaariy na Muslim ilhali hiyo Hadiyth nyingine inamwendea Ibn Abiy Shaybah (12/110/2. Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (8).

[3] Bi maana daima nakutii, nakutumikia na kufuata dini Yako unayoiridhia.

[4] Shari hainasibishwi na Allaah (Ta´ala) kwa kuwa katika matendo Yake (Ta´ala) hakuna shari. Matendo Yake yote (´Azza wa Jall) ni kheri kwa kuwa yamejengwa juu ya uadilifu, fadhila na hekima. Yote ni kheri na hakuna shari ndani yake. Shari imekuwa shari kwa kuwa haziegemezwi Kwake (Ta´ala). Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ameumba (Subhaanah) kheri na shari. Shari inapatikana katika baadhi ya viumbe Wake na si katika uumbaji wala matendo Yake. Kwa ajili hii ndio maana (Subhaanah) amejikatasa kutokamana na dhuluma ambayo maana yake ni kuyaweka mambo pasipokuwa mahala pake. Hayaweki mambo isipokuwa mahala pake stahiki. Hiyo ni kheri tupu. Shari inahusiana na kuyaweka mambo pasipokuwa mahala pake. Akiyaweka mahala pake stahiki haiwi shari. Kwa hiyo tumejua kuwa shari haitoki Kwake… Ukiuliza ni kwa nini ameumba shari, viumbe ni Vyake na matendo Yake ni kheri na si shari. Ummbaji na kitendo vimesimama kupitia Yeye (Subhaanah) kinyume na shari haiwezekani kabisa kusimamishwa Naye na kuegemezewa nayo. Shari inayopatikana katika viumbe haiegemezwi na kunasibishwa Kwake. KItendo na uumbaji vinanasibishwa Kwake na ndio maana ni kheri.” Tazama zaidi utafiti huu katika kitabu chake “Shifaa’-ul-Ghaliyl”, uk. 178-206.

[5] Muslim, Abuu ´Awaanah, Abuu Daawuud, an-Nasaa’iy, Ibn Hibbaan, Ahmad, ash-Shaafi´iy na at-Twabaraaniy. Mwenye kudai kuwa Hadiyth inahusiana tu na swalah ya sunnah amekosea.

[6] an-Nasaa’iy kwa isnadi nzuri.

[7] an-Nasaa’iy na ad-Daaraqutwniy med kwa isnadi nzuri.

[8] Bi maana nakutakasa kutokamana na mapungufu yote.

[9] Bi maana ni nyingi baraka ya jina Lako kwa vila kila mwenye kulitaja anapata baraka.

[10] Bi maana utukufu na ukubwa Wako uko juu kabisa.

[11] Abuu Daawuud na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. al-´Uqayliy amesema:

”Imepokelewa kupitia njia mbalimbali kwa isnadi nzuri.” (uk. 103) Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (341).

[12] Ibn Mandah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (2/123) kwa isnadi Swahiyh. Ameipokea an-Nasaa’iy katika ”al-Yawm wal-Laylah” kutoka kwa Swahabah na kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama alivyotaja Ibn Kathiyr katika ”Jaami´-ul-Masaaniyd” (2/235/2/3). Nimeikuta kwa an-Nasaa’iy (849, 850) na nimeitaja katika ”as-Swahiyhah” (2939).

[13] Abuu Daawuud na at-Twahaawiy kwa isnadi Swahiyh.

[14] Muslim na Abuu ´Awaanah.

[15] al-Bukhaariy, Muslim, Abuu ´Awaanah, Abuu Daawuud, Ibn Naswr na ad-Daarimiy.

[16] Hii haina maana kabisa kwamba haikuwekwa katika Shari´ah kuisoma katika swalah za faradhi. Isipokuwa tu imamu asiisomi kwa kukhofia asije kuwarefushia swalah maamuma.

[17] Ahmad, Ibn Abiy Shaybah (2/119/12), Abuu Daawuud na at-Twabaraaniy katika ”al-Awsat” (2/62) kwa isnadi Swahiyh na nzuri iliyopo katika ”as-Swaghiyr” yake.

[18] at-Twayaalisiy na Abuu Daawuud kwa isnadi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 80-83
  • Imechapishwa: 13/10/2016