16. Macho yanatakiwa kuangalia mahala pa kusujudia na unyenyekevu katika swalah

16- Alipokuwa anaswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alikuwa akiinamisha kichwa chake na akiangalia ardhini[1].

Alipoingia Ka´bah macho yake hayakuacha mahala anaposujudia mpaka alipotoka[2].

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyumbani hakutakiwi kuwa kitu kinachomshughulisha mswaliji.”[3]

Amekataza mtu kutazama mbinguni[4].

Amesisitiza makatazo na kusema:

“Waache wale wanaonyanyua macho yao juu katika swalah au hayatowarudilia.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… au wayakose.”[5]

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Mnaposwali msiangaze, kwani hakika Allaah anauelekeza uso Wake mbele ya uso wa mja Wake maadamu haangazi kwengine.”[6]

Amesema vilevile kuhusu kuangaza huku na kule:

“Ni unyakuaji ambao shaytwaan ananyakua swalah ya mja.”[7]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah haachi kuwa mbele ya yule mwenye kuswali midhali haangazi huku na kule. Anapougeuza uso wake Anaondoka kutoka kwake.”[8]

Amekataza mambo matatu; kudonoa kama anavyodonoa jogoo, kukaa kama anavyokaa mbwa na kuangaza kama mbweha[9].

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swali swalah ya kuaga kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona.”[10]

Amesema pia:

“Hakuna mtu anayeswali swalah ya faradhi pindi wakati wake unapoingia, akatawadha vizuri, akawa na unyenyekevu na kurukuu´ vizuri, isipokuwa inakuwa ni kafara ya madhambi yake yaliyotangulia isipokuwa yale makubwa – hili linahusu mwaka mzima.” Muslim.

Aliswali (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenye Khamiyswah[11] iliyo na mifumo na akatazama mifumo yake. Alipomaliza akasema:

“Ipelekeni kanzu hii kwa Abu Jahm na mniletee Anbajaaniyah[12] ya Abu Jahm. Inanishughulisha kutokamana na swalah yangu.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Kwani nimetazama mifumo yake katika swalah na imekaribia kunitia katika mtihani.”[13]

´Aaishah alikuwa na kitambaa cha mapicha kilichotandazwa mpaka kwenye Sahwah[14] ambacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali kukielekea. Kisha akasema:

“Kiondoeni kwangu [kwani kila mara ninaona mapicha yake mbele yangu ninaposwali].”[15]

Alikuwa akisema:

“Kusiswaliwe pindi chakula kimeshatengwa au pindi mtu anapohitajia kufanya haja mbili.”[16]

[1] al-Bayhaqiy na al-Haakim aliyesema kuwa ni Swahiyh, na ni kweli. Hadiyth hii ina upokezi unaoitilia nguvu kutoka kwa Maswahabah kumi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na imepokelewa na Ibn ´Asaakir (17/202/2). Tazama””al-Irwaa’” (354).

[2] al-Bayhaqiy na al-Haakim aliyesema kuwa ni Swahiyh, na ni kweli.

[3] Abuu Daawuud na Ahmad kwa isnadi Swahiyh.

[4] al-Bukhaariy na Abuu Daawuud.

[5] al-Bukhaariy, Muslim na as-Siraaj.

[6] at-Tirmidhiy na al-Haakim aliyesema kuwa ni Swahiyh. Swahiyh at-Targhiyb (353).

[7] al-Bukhaariy na Abuu Daawuud.

[8] Abuu Daawuud na wengineo. Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan. Swahiyh at-Targhiyb (555).

[9] Ahmad na Abuu Ya´laa. (Swahiyh at-Targhiyb (556).

[10] al-Mukhallasw i ”Ahaadiyth Muntaqaat, at-Twabaraaniy, ar-Rawayaaniy, adh-Dhwiyaa’, Ibn Maajah, Ahmad na Ibn ´Asaakir. Swahiyh kwa mujibu wa Faqiyh al-Haythamiy katika “Asnaa al-Matwaalib””.

[11] Nguo ya pamba iliyofumwa.

[12] Nguo pana ambayo haikufumwa.

[13] al-Bukhaariy, Muslim na Maalik. Imetajwa katika ”al-Irwaa’”’” (376).

[14] Kijumba kidogo kilichofukiwa kidogo ardhini na kimeshabihiana na chumba cha kulalia au chumba cha kuhifadhia vitu. (an-Nihaayah)

[15] al-Bukhaariy, Muslim na Abuu ´Awaanah. Sababu – na Allaah ndiye mwenye kujua zaidi – ya ni kwa nini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuamrisha mapicha yachanwe na badala yake akatosheka na kuyaondo, ni kwa sababu hayakuwa na roho. Dalili ya hilo ni kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyachana mapicha mengine, kama ilivyotajwa katika mapokezi katika al-Bukhaariy na Muslim. Anayetaka kutafiti haya zaidi arejee katika “Fath-ul-Baariy” (10/321) na ”Ghaayat-ul-Maraam fiy Takhriyj Ahaadiyth al-Halaal wal-Haraam ”(131-145).

[16] al-Bukhaariy na Muslim ilihali hiyo Hadiyth nyingne inamwendea Ibn Abiy Shaybah (12/110/2). Imetajwa katika ”al-Irwaa’” (8).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 78-80
  • Imechapishwa: 13/10/2016