17. Allaah ametakasika na mapungufu na kasoro aina zote

Na Yeye (Subhaanah) kwa yale aliyojisifia na kujiita kwayo… Amekusanya kati ya upambanuzi katika kuthibitisha na ujumla katika ukanushaji pale aliposema:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja Pekee. Allaah ambaye ni Mwenye kukusudiwa. Hakuzaa na wala Hakuzaliwa. Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.”(112:01-04)

Amesema kuwa Yeye ndiye Allaah, Mmoja Pekee na ndiye Mwenye kukusudiwa. Halafu akasema:

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ

Hakuzaa na wala Hakuzaliwa.”

Huu ni ufafanuzi maalum ambapo ndani yake amekanusha kuwa na mwana, kwa sababu jambo hilo linapelekea katika mapungufu. Kisha akasema (Ta´ala):

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)

Ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye Jina kama Lake?” (19:65)

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye [washirika] na hali ya kuwa nyinyi mnajua [kuwa hana].” (02:22)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Dalili ya Uhai wa Allaah

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ

“Allaah, hakuna mungu wa haki ila Yeye – Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu. Haumchukuwi usingizi wala kulala.” (02:255)

Amejikanushia kuchukuliwa na usingizi na kulala. Usingizi ni mzito zaidi kuliko kulala. Amejikanushia haya kwa sababu Yeye (Subhaanah) anasifika kuwa na uhai ulio mkamilifu. Kwa sababu ulalaji na usingizi ni upungufu katika uhai. Kwa ajili hiyo Allaah akawa ni mwenye kutakasika na hayo. Yeye ni ambaye yuhai na hafi. Kulala ni aina ya kufa. Hakika Yeye (Subhaanah) yuhai na hafi.

لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

“Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi.”

Bi maana Yeye ndiye mfalme wa kila kitu.

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake.

Bi maana hakuna yeyote atayeombea mbele Yake siku ya Qiyaamah isipokuwa kwa idhini Yake. Mitume na waja wema wataombea baada ya kupata idhini Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kuhusiana na duniani Allaah (Subhaanah) amewaamrisha watu wote wamuombee Yeye Pekee du´aa na wawaombee uombezi ndugu zao duniani kwa ajili ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaombea pindi anapotakwa uombezi. Pindi mmoja katika watu anapomuomba uombezi na amtatulie tatizo anamuombea (´alayhis-Swalaatu was-Salaam)[1].

Kuhusiana na siku ya Qiyaamah hakuna yeyote atayeombea uombezi isipokuwa kwa idhini Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Ama duniani wanaombea kwa idhini Yake ya kijumla. Kwa sababu ameidhinisha katika Shari´ah waumini kuombeana idhini kati yao. Amesema (Ta´ala):

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا

“Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake, na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu yake.” (04:85)

Amewaidhinisha (Subhaanah) na kuwasisitiza kufanya hivo; wasaidiane katika wema na uchaji Allaah, wapeana nasaha na kuusiana kwa haki. Uombezi unaingia katika kuusiana kwa haki na ni katika kufanya wema. Uombezi unajuzu duniani kwa idhini Yake (Subhaanah) ya kijumla. Ama kuhusu Aakhirah uombezi hautofaa isipokuwa baada ya kupata idhini Yake maalum. Hakuna yeyote atayeombea isipokuwa kwa idhini Yake (Subhaanah). Kwa ajili hii watu siku ya Qiyaamah watamwendea Aadam, Nuuh, Ibraahiym na Muusa, ´Iysaa (´alayhimus-Salaam) ambapo wote wataomba udhuru. Hatimaye waende kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asujudu mbele ya Mola Wako chini ya ´Arshi, kisha amhimidi Allaah kwa himdi kubwa na halafu baada ya hapo ndio ampe idhini na kumwambia:

“Ombea utapewa.”

Aayah hii ambayo ni Aayat al-Kursiy ndio Aayah kubwa katika Qur-aan. Ndani yake mna uthibitisho na ukanushaji:

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ

“Allaah, hakuna mungu wa haki ila Yeye – Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu.”

Huu ni uthibitisho.

لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ

“Haumchukuwi usingizi wala kulala.”

Huu ni ukanushaji.

لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

“Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi.”

Huu ni uthibitisho.

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai [anayeombea] mbele Yake bila ya idhini Yake.”

Huu ni uthibitisho.

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ

“Anajua yaliyo mbele yao [viumbe] na yaliyo nyuma yao.”

Huu ni uthibitisho.

وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Wala hawakizunguki chochote kile katika Elimu Yake isipokuwa kwa Alitakalo. Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye mkuu.”(02:255)

Amebainsiha ukamilifu Wake na kwamba Yeye ni ndiye aliye juu na mkuu na kwamba Yeye ana uhai mkamilifu na kwamba Yeye ni aliye hai na kwamba ndiye Msimamizi wa kila kitu na kwamba Yeye ndiye Mwenye kumiliki kila kitu. Lililo la wajibu ni kunyenyekea Kwake na kumuomba (Subhaanahu wa Ta´ala) na kumwelekea katika kila jambo. Mambo yote yanapitika kupitia Mikono Yake. Ndio maana amesema (Subhaanah):

ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

“Niombeni, Nitakuitikieni.” (40:60)

وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ

“Na muombeni Allaah fadhila Zake.” (04:32)

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi Niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.” (02:186)

[1] Tazama al-Bukhaariy (5652) na Muslim (2576).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com