18. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan II

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Subhaanah):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Yeye Ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye Karibu, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi.” (57:03)

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ

”Na mtegemee Aliye hai Ambaye Hafi.” (25:58)

وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

”Naye Ndiye Mjuzi, Mwenye hikmah.” (66:02)

وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye ndiye Mwenye hikmah, Mjuzi.” (06:18)

يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا

”Anajua yale yote yanayoingia ardhini na yale yote yanayotoka humo, na yale yote yanayoteremka kutoka mbinguni na yale yote yanayopanda huko.” (34:02)

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

”Na Kwake Pekee zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua. Na wala [haianguki] punje katika viza vya ardhi, na wala [hakianguki] kilichorutubika na wala [hakianguki] kikavu isipokuwa [kimeandikwa] katika Kitabu kinachobainisha.” (06:59)

وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ

“Na mwanamke yeyote yule habebi [mimba] na wala hazai isipokuwa kwa ujuzi Wake.” (35:11)

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”Ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi.” (65:12)

إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

”Hakika Allaah Ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu kali madhubuti.” (51:58)

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye Ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا

”Hakika [mawaidha] Anayokuwaidhini nayo Allaah ni mazuri kabisa; hakika Allaah ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (04:58)

وَلَوْلَا إِذْ دَخَلْتَ جَنَّتَكَ قُلْتَ مَا شَاءَ اللَّـهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِاللَّـهِ

“Na lau ulipoingia bustanini mwako ungelisema: “Ametaka Allaah; hapana nguvu ila kwa Allaah.” (18:39)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana lakini Allaah Anafanya Ayatakayo.” (02:153)

أُحِلَّتْ لَكُم بَهِيمَةُ الْأَنْعَامِ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ غَيْرَ مُحِلِّي الصَّيْدِ وَأَنتُمْ حُرُمٌ ۗ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ

”Imehalalishwa kwenu wanyama wenye miguu minne isipokuwa mnaosomewa [kuwa ni haraam]. Lakini msihalalishe kuwinda hali mkiwa katika Ihraam. Hakika Allaah Anahukumu Atakayo.” (05:01)

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ

”Basi yule ambaye Allaah Anataka kumwongoza, Humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule ambaye Anataka kumpoteza Humjaalia kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana kama kwamba anapanda mbinguni kwa tabu.” (06:125)

MAELEZO

Aayah hizi Allaah amekusanya ndani yake yale aliyojiita na kujisifu kwayo Mwenyewe baina ya ukanushaji na uthibitisho. Allaah anathibitishiwa sifa kamilifu na anakanushiwa sifa zilizo na mapungufu na aibu. Tumetangulia kuizungumzia Aayat al-Kursiy na Suurah “al-Ikhlaasw” na faida zinazopatikana ndani yake. Amesema (Ta´ala):

Dalili kwamba Allaah ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

”Yeye Ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye Karibu, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi .”(57:03)

Amethibitisha (Subhaanah) ya kwamba Yeye ni wa Mwanzo ambaye hakuna kitu kabla Yake. Hivyo ndivyo amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Allaah! Hakika Wewe ndiye wa Mwanzo na hakuna kitu kabla Yako, Wewe ndiye wa Mwisho na hakuna kitu baada Yako, Wewe ndiye ulie Juu na hakuna kitu juu Yako.”[1]

adhw-Dhwaahir [Aliye juu], bi maana Yeye ndiye Yuko juu ya viumbe vyote. Kwa msemo mwingine hakuna kitu kilicho juu Yake.

al-Baatwin [Aliye karibu], bi maana hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye. Kwa msemo mwingine anakijua kila kitu. Hakuna chenye kufichikana Kwake.

Kadhalika Aayah nyienginezo baada yake zinazozungumzia juu ya Ujuzi:

وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ

”Naye Ndiye Mjuzi, Mwenye hikmah.”(66:02)

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”Ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah Amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi.”(65:12)

Vilevile Aayah nyenginezo ambazo zimetaja Ujuzi na hekima. Kwa mfano:

إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah.” (02:220)

Aayah zilizotaja riziki na nguzu. Kwa mfano:

Dalili ya Nguvu na Kuruzuku kwa Allaah

إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

”Hakika Allaah Ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu kali madhubuti.”(51:58)

Aayah zilizotaja utashi, matakwa na kadhalika. Zote hizi zinaonyesha ukubwa Wake (Subhaanah), kwamba Yeye ana utashi kamilifu, matakwa kamilifu, elimu kamilifu na uwezo kamilifu. Zote hizi ni sifa Zake (Jalla wa ´Alaa). Lakini hata hivyo zinatakiwa kuthibitishwa kwa njia isiyofanana na viumbe. Bi maana Ana nguvu lakini sio kama nguvu za viumbe. Yeye nguvu Zake ni kamilifu kabisa. Vivyo hivyo inahusiana na sifa Zake zingine zote. Siza Zake zote ni kamilifu. Kwa ajili hii ndio maana amesema:

Dalili ya Allaah kutolingana na chochote na kuwa na mwenza

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.” (42:11)

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ

“Basi msimpigie mifano!” (16:74)

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye Jina kama Lake?” (19:65)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)

Elimu Yake ni kamilifu na sio kama elimu ya viumbe. Hakuna chochoye chenye kufichikana Kwake. Vivyo hivyo hekima Yake, uwezo Wake, nguvu Zake, upole Wake, usikizi Wake na uoni Wake. Zote hizi ni sifa kamilifu. Sifa hizi hazina upungufu wowote ndani yake. Hili ni tofauti na sifa za viumbe ambapo zina upungufu na ni dhaifu. Kuhusu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) sifa Zake zote ni kamilifu. Amesema (Ta´ala):

Dalili ya Kuona na Kusikia kwa Allaah

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye Ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Hili ni kutokana na ukamilifu Wake:

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye Jina kama Lake?” (19:65)

Kwa msemo mwingine hana samiya mwenye kulingana Naye kutokana na ukamilifu Wake.

Dalili ya Utashi na Matakwa ya Allaah

Vilevile Allaah anasifika kuwa na matakwa. Maana yake ni utashi wa kilimwengu. Kwa msemo mwingine matakwa Yake ni yenye kutendeka na hayarudishwi/hayazuiwi na kitu. Kile anachotaka Allaah ndio huwa, sawa iwe ni mauti, uhai, kuwafanya watu fulani wawe na nguvu, kuwafanya watu wengine wawe madhalili, kuwaondoshea watu fulani ufalme, kuwafanya watu fulani wawe na ufalme, kuwafanya watu fulani wapate watoto au kutowapata. Yote hayo ni yenye kutendeka pale Allaah anapotaka. Amesema (Ta´ala):

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke. Na hamtotaka isipokuwa Atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:28-29)

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ

“Na lau Angetaka Mola wako wasingeliyafanya hayo.” (06:112)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا

“Na lau Angelitaka Allaah wasingelipigana.” (02:253)

[1] Muslim (2713).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com