Kuna aina mbili za Utashi:

1- Utashi wa kilimwengu (Kawniyyah). Utashi wa kilimwengu ni kama matakwa. Utashi aina hii ni wenye kutekelezwa na haurudishwi na kitu. Mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن يُرِدِ اللَّـهُ أَن يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَن يُرِدْ أَن يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ

”Basi yule ambaye Allaah Anataka kumwongoza, Humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule ambaye Anataka kumpoteza Humjaalia kifua chake kuwa na dhiki chenye kubana kama kwamba anapanda mbinguni kwa tabu.”(06:125)

إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ

“Hakika Allaah Anahukumu Atakayo.” (05:01)

Huu ni utashi wa kilimwengu wenye kutendeka. Ni kama mfano wa matakwa. Haurudishwi na kitu.

2- Utashi wa kidini (Shar´iyyah). Utashi aina hii maana yake ni kupenda na kuridhia. Utashi huu unaweza kutokea na huenda vilevile usitokee. Mfano wa Kauli Yake (Ta´ala):

يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ وَاللَّـهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيْكُمْ

“Allaah Anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za wale walio kabla yenu na Apokee tawbah kwenu. Na Allaah Mjuzi, Mwenye hikmah. Na Allaah Anataka kupokea tawbah kwenu.” (04:26-27)

Huu ni utashi wa kidini. Unaweza kutokea kama ambavyo vilevile huenda usitokee. Allaah anapenda awaongoze waislamu wote. Allaah anapenda awasamehe. Huu ni utashi wa kidini. Viumbe wengi hawakusamehewa. Viumbe wengi wamekufa juu ya kufuru. Utashi wa kidini unaweza kutokea kama ambavyo vilevile huenda usitokee.

Allaah amependa kidini wanaadamu wakubali haki, wawafuate Mitume na wamtii Allaah. Pamoja na hivyo kuko miongoni mwao ambao wamemtii na wengine wakamuasi. Mwenye kumtii ana Pepo na mwenye kumuasi ana Moto. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na yeyote atakayemtii Allaah na Mtume Wake Atamuingiza katika Pepo zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo – na huko ndiko kufuzu kukubwa kabisa. Na yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake na akapindukia mipaka Yake Atamuingiza Motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha.” (04:13-14)

Wote wamepewa matishio. Mwenye kutii kwa khiyari na kutaka kwake basi ana Pepo. Na yule mwenye kuasi ana Moto. Huu ni utashi wa kidini.

Kuhusiana na utashi hakuna yeyote anaweza kuukwepa. Yale anayotaka Allaah yatokee katika ulimwengu ni lazima yatokee. Kwa mfano Allaah anapotaka kuwaangamiza watu fulani, kuwafanya wawe na nguvu, kumfisha fulani, kumpa uhai, kumhuisha fulani, kumfanya akabaki na mengineyo. Utashi wa kilimwengu ni kama mfano wa matakwa. Matakwa yake ni lazima yatendeke.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com