20. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan III

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala):

وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

”Na fanyeni wema, Hakika Allaah Anapenda watendao wema.” (02:195)

وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

”Na fanyeni haki. Hakika Allaah Anapenda wafanyao haki.” (49:09)

فَمَا اسْتَقَامُوا لَكُمْ فَاسْتَقِيمُوا لَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ

”Basi wakikunyokeeni [kwa uzuri], nanyi wanyokoeeni [kwa uzuri]. Hakika Allaah Anapenda wamchao.” (09:07)

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

”Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni, Atakupendeni Allaah.” (03:31)

فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ

”Basi Allaah Ataleta watu [badala yao] Atakaowapenda nao watampenda.” (05:54)

إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِهِ صَفًّا كَأَنَّهُم بُنْيَانٌ مَّرْصُوصٌ

”Hakika Allaah Anapenda wale wanaopigana katika njia Yake safu kwa safu kama kwamba wao ni jengo linalokamatana barabara.” (61:04)

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ

“Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye mapenzi halisi.” (85:14)

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

”Kwa Jina la Allaah Mwingi wa Rahmah, Mwenye kurehemu.” (27:30)

رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا

“Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa Rahmah na elimu.” (40:07)

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“Naye daima kwa Waumini ni Mwenye kuwarehemu.” (33:43)

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ

“Na Rahmah Yangu imeenea kila kitu.” (07:156)

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ

Mola wenu Amekidhia juu ya Nafsi Yake Rahmah.” (06:54)

وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

”Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (10:107)

فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُالرَّاحِمِينَ

”Basi Allaah ni Mbora wa kuhifadhi, Naye ni Mbora wa kurehemu kuliko wanaorehemu.” (12:64)

رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

”Allaah Ataridhika nao, nao wataridhika Naye.” (98:08)

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

”Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni [Moto wa] Jahannam, atadumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu.”(04:93)

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّـهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ

”Hivyo kwa kuwa wao wamefuata yale yanayomghadhibisha Allaah, na wakachukia radhi Zake, basi Akazibatilisha ‘amali zao.” (47:28)

فَلَمَّا آسَفُونَا انتَقَمْنَا مِنْهُمْ

”Basi walipotukasirisha; Tuliwapatiliza.” (43:55)

وَلَـٰكِن كَرِهَ اللَّـهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ

”Lakini Allaah Amechukia kutoka kwao, basi Akawazuia.” (09:46)

كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

”Ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.” (61:03)

MAELEZO

Aayah hizi nyingi ndani yake mna sifa ya kupenda. Allaah amejisifu Mwenyewe kwa sifa ya kupenda, kwamba anapenda na kupendwa na kwamba anawapenda wachaji Allaah, watendao wema, wafanyao uadilifu. Amesema (Ta´ala):

Dalili ya Kupenda kwa Allaah

فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ

”Basi Allaah Ataleta watu [badala yao] Atakaowapenda nao watampenda.”(05:54)

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

”Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni, Atakupendeni Allaah.” (03:31)

Vilevile Yeye ni Mwingi wa rehema, mwenye kurehemu; Yeye ni mwenye huruma, huruma Wake umeenea kwenye kila kitu, Yeye ni mwenye kusamehe, mwenye mapenzi, huridhia, hughadhibika, huchukia na hukirihika:

Dalili ya Kuridhia na Kughadhibika kwa Allaah

رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

”Allaah Ataridhika nao, nao wataridhika Naye.” (98:08)
 

غَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِم

 
  “Allaah Ameghadhibika nao.” (48:14)  

اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّـهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ

“Wamefuata yale yanayomghadhibisha Allaah na wakachukia radhi Zake.” (47:28)

وَلَـٰكِن كَرِهَ اللَّـهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ

”Lakini Allaah Amechukia kutoka kwao, basi Akawazuia.” (09:46)

Zote hizi ni sifa za haki. Radhi, mapenzi, kukasirika na kuchukia. Zote hizi anasifiwa nazo (Jalla wa ´Alaa). Ni kama sifa nyenginezo ambazo zinalingana na Allaah peke Yake. Mtu anatakiwa kuzithibitisha bila ya kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna na kuzipigia mfano. Kupenda Kwake sio kama wanavyopenda viumbe, kuridhia Kwake sio kama kuridhia kwa viumbe, kuchukia Kwake sio kama wanavyochukia viumbe. Vivyo hivyo inahusiana na sifa nyenginezo. Mlango ni ule ule mmoja. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye Ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)
 

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

 
  “Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)  

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

 
”Basi msipigie mifano Allaah! Hakika Allaah Anajua nanyi hamjui.” (16:74)  

Bi maana hana anayefanana Naye. Usimpigie Allaah mifano. Kwani Allaah hana mwenza na hana mshirika. Sifa zote mlango wake ni ule ule mmoja: tunasema kuwa tunamuamini Allaah (Jalla wa ´Alaa) na majina Yake mazuri na sifa Zake kuu zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah Swahiyh kwa njia inayolingana na Allaah. Tunafanya hivyo pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna na kuzilinganisha. Badala yake tunasema kuwa sifa Zake zote ni haki na majina Yake yote ni mazuri. Tunamthibitishia nayo Allaah kama ambavyo Yeye Mwenyewe (Jalla wa ´Alaa) amevyojithibitishia nayo, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Wameyathibitisha kwa njia inayolingana na Yeye. Sifa Zake hazifanani na sifa za viumbe Wake. Majina Yake hayafanani na majina ya viumbe. Yeye (Subhaanah) ana majina mazuri na yana maana kuu. Kwa ajili hii amesema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

“Na Allaah Ana Majina mazuri kabisa, basi muombeni kwayo.” (07:180)

Hili ni kutokana na ukamilifu Wake na ukamilifu wa maana yake. Ndio maana Akayaita (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwa ni majina mazuri kabisa.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com