Kadhalika kurudisha kwao maoni yanayokwenda kinyume na Sunnah yalikuwa ni mafupi yenye kutosheleza lakini pia kwa ibara zilizo nzuri kabisa. Yule mwenye kuyafahamu hahitajii maneno yaliyorefushwa ya wanafalsafa waliokuja baadaye. Bali ukweli wa mambo ni kwamba pengine maneno yao marefuya waliokuja baada yao yakakosa usawa uliokuweko katika maneno ya Salaf na maimamu licha ya ufupi wake. Wale Salaf walionyamaza na kuepuka magomvi hawakufanya hivo kutokana na ujinga na kushindwa, lakini ilikuwa ni kutokana na elimu na kumcha Allaah. Wale waliokuja nyuma ambao walizungumza na kuingia kwa undani hawakufanya hivo kwa sababu eti walijua kitu ambacho hakikujulikana na wale wa mwanzo, lakini walifanya hivo kwa sababu ya kupenda kuongea na uchache wa kumcha Allaah. Kama alivosema al-Hasan pindi alipowasikia watu wanajadili:

“Hawa ni watu ambao ´ibaadah zimewachosha, wamechukulia sahali kuongea na kumekuwa kuchache kumcha kwao Allaah. Ndio maana wakazungumza.”

Mahdiy bin Maymuun amesema:

“Muhammad bin Siyriyn alimwona mtu mmoja akasema: “Mimi najua anachokitaka. Lau ningelitaka kubishana nawe basi ningekuwa mwanachuoni katika mambo ya ubishi.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mimi ni mjuzi wa kubisha zaidi yako, lakini sitaki kubishana nawe.”

Ibraahiym an-Nakha´iy amesema:

“Sijapatapo kugombana.”

´Abdul-Kariym al-Jazariy amesema:

“Mchaji hajapatapo kugombana.”

Ja´far bin Muhammad amesema:

“Tahadharini na mambo ya kugombana katika dini. Kwani ni mambo yanaushughulisha moyo na kurithisha unafiki.”

´Umar bin ´Abdil-´Aziyz alikuwa akisema:

“Ukisikia mivutano basi jitenge mbali.”

Amesema tena:

“Yule mwenye kuifanya dini yake ni lengo la mivutano basi anakuwa ni mwenye kuhamahama kwa wingi.”

 Amesema tena:

“Wale wa mwanzo walisimama kwa utambuzi na walijizuia kutokana na uoni wa mbali, licha ya kwamba walikuwa na nguvu ya kutafiti.”

Maneno ya Salaf katika mada hii ni mengi sana.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 60-62
  • Imechapishwa: 21/09/2021