Wengi katika wale waliokuja nyuma wamepewa mtihani kwa jambo hili. Wamedhani kuwa yule mwenye kuzungumza, akajadili na akagombana sana katika mambo ya dini basi ndiye mjuzi zaidi kuliko yule asiyefanya hivo. Fikira ambayo ni ujinga mtupu. Watazame wale Maswahabah wakubwa na mabingwa wao kama mfano wa Abu Bakr, ´Umar, ´Aliy, Mu´aadh, Ibn Mas´uud na Zayd bin Thaabit – walikuweje? Maneno yao ni machache kuliko ya Ibn ´Abbaas, ingawa ni wajuzi zaidi kumliko. Maneno ya Taabi´uun ni mengi zaidi kuliko ya Maswahabah, licha ya kuwa Maswahabah walikuwa wajuzi zaidi kuwaliko. Kizazi cha wale waliokuja baada ya Taabi´uun maneno yao yalikuwa mengi zaidi kuliko maneno ya Taabi´uun, ingawa Taabi´uun walikuwa ni wajuzi zaidi kuwaliko. Kwa hivyo elimu haihusiani na kupokea mapokezi au nukuu nyingi; lakini elimu ni nuru inayowekwa ndani ya moyo ambayo inamfanya mja kuifahamu haki. Inamfanya kuweza kupambanua kati ya haki na batili na baadaye anaiabiri kwa ibara na jumla fupi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizawadiwa maneno kama hayo; alikuwa akizungumza maneno mafupi, lakini yenye maana pana. Kwa ajili hiyo ndio maana kumepokelewa makatazo ya kuzungumza sana na kuleta porojo nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hakumtuma Mtume isipokuwa kwa njia ya kufikisha. Hakika kujikakama kwa maneno kunatokamana na Shaytwaan.”[1]

Hiyo ina maana kwamba Mtume huzungumza kwa kile kiasi anachohitajia kwa ajili ya kufikisha ujumbe. Kuhusu maneno na kujikakama kwa wingi ni jambo linalosimangwa. Khutbah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zilikuwa fupi[2]. Akizungumza basi mtu alikuwa anaweza kuyahesabu maneno yake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika si venginevyo hakika miongoni mwa ubainifu uko ambao ni uchawi.”[3]

Alisema hivo kwa njia ya kusimanga na si kwa njia ya kusifia, kama walivyofikiria baadhi ya watu. Yule ambaye atazingatia mtiririko wa matamshi ya Hadiyth basi atayakinisha jambo hilo. at-Tirmidhiy na wengine wamepokea kwamba ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anawabughudhi wanamme wenye balagha na wenye kujikakama ambao wanavingirisha ndimi zao kama ambavo ng´ombe anavingiriza ulimi wake.”[4]

Yako maneno mengi mfano wa hayo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Maswahabah kama vile ´Umar, Sa´d, Ibn Mas´uud na ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhum). Hiyo ina maana kwamba si kila ambaye anazungumza na kuandika sana mambo ya kielimu eti ni mjuzi zaidi kuliko ambaye hafanyi hivo.

[1]´Abdur-Razzaaq (11/163-164).

[2]Muslim (2/591).

[3]al-Bukhaariy (5146) na Muslim (869).

[4]Ibn Abiy Shaybah (6348), Ahmad (6543), Abu Daawuud (5005), at-Tirmidhiy (2853), Ibn Abiy Haatim katika ”al-´Ilal” (2547).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 62-65
  • Imechapishwa: 21/09/2021