´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 2: Ni nini imani na Uislamu na ni ipi misingi yake?

Jibu: Imani ni usadikishaji wa kukata kabisa yale yote ambayo Allaah na Mtume Wake wameamrisha kuyasadikisha. Usadikishaji wa kukata huo ndani yake mna kitendo. Kitendo hicho ndio Uislamu ambao maana yake yake ni kujisalimisha kwa Allaah peke yake na kunyenyekea Kwake kwa kumtii.

Kuhusiana na misingi yake ni ile ilio katika Aayah hii tukufu ifuatayo

قُولُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُون

”Semeni: “Tumemwamini Allaah na yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na al-Asbaatw na aliyopewa Muusa na ‘Iysaa na waliyopewa Manabii kutoka kwa Mola wao, hatutofautishi baina ya mmoja yeyote miongoni mwao nasi Kwake tunajisalimisha.” (02:136)

Katika hiyo kunaingia pia yale aliyofasiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Jibriyl na wengine pale aliposema:

”Imani kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar; kheri na shari yake.”

Amesema pia:

”Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa yule mwenye kuweza kufanya hivo.”[1]

MAELEZO

Uislamu na imani kinapotajwa kila kimoja peke yake basi kimoja kinaingia ndani ya kingine. Ama vinapotajwa kwa pamoja, kama ilivyo katika Hadiyth ya Jibriyl, basi katika hali hiyo Uislamu unakuwa na maana ya zile nguzo tano, zinazotambulika na zilizowazi na imani inakuwa na maana ya zile i´tiqaad zilizojificha. Kila kimoja kinaingia ndani ya kingine kwa njia fulani.

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

”Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga ramadhaan na kuhiji Nyumba kwa yule mwenye kuweza kufanya hivo.”

Haya yanapelekea kuamini yale yote yaliyokusanywa na shahaadah. Mja anaingia ndani ya Uislamu kwa kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Yeyote ambaye hakubali Shahaadah mbili hizi basi hawi muislamu na hajaingia katika Uislamu. Shahaadah ndio funguo ya Uislamu na ya imani. Kupitia Shahaadah ndio kunatimia mafungamano pamoja na Allaah (´Azza wa Jall) ambapo mja atamwabudu Allaah (Subhaanah) pekee kwa mujibu wa yale aliyoyaweka katika Shari´ah ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu nguzo zingine zilizobaki ni za kimatendo.

Swalah ndio nguzo ya pili na inahusiana na mwii ukishirikiana na ulimi, moyo na viungo vya mwili.

Zakaah imefungamana na mali. Mja atekeleze zile faradhi ambazo Allaah amemfaradhishia za aina mbalimbali ya mali. Ni mamoja inahusu zakaah ya nafaka, mifugo, pesa au bidhaa za biashara.

Kufunga Ramadhaan ndio nguzo ya tano na inahusiana na mtu kujizuia kutokamana na kula, kunywa, jimaa na vitangulizi vyake kuanzia pale kunapochomoza alfajiri mpaka jua kuzama. Faradhi hii imefungamana na shahawa tatu; chakula, kinywaji na jimaa. Anapaswa kujizuia na mambo hayo kwa ajili ya kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall) na kwa mujibu wa Shari´ah ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Nguzo ya sita ni kuhiji Nyumba ya Allaah tukufu mara moja katika umri. Vivyo hivyo inahusiana na ´Umrah.

Ama kuhusu imani, nguzo zake ni sita na zote zinahusiana na mambo ya kuamini.

Ya kwanza ni kumwamini Allaah ikiwa na maana ya kuamini uwepo Wake na uwezo Wake juu ya kila kitu, anajua kila kitu na anaumba na kuendesha kwa hekima Yake na yale yanayohusiana na hayo miongoni mwa sifa za Allaah (´Azza wa Jall)  zinazolingana na utukufu Wake.

Inatakiwa vilevile kuamini mbingu saba na wale Malaika waliyomo ndani yake na ardhi saba na vile vyote vilivyomo ndani yake kwamba ni milki ya Allaah (´Azza wa Jall). Yeye ndiye Mwenye kuviendesha na kwamba dunia ni nyumba ya mitihani. Allaah anampa mtihani mja Wake kwa utajiri na ufukara, uhai na kifo, afya njema na maradhi, imani na ukafiri.

Inatakiwa vilevile kuamini kwamba kufufuliwa baada ya kufa ni jambo halina shaka kabisa. Baada ya kufufuliwa viumbe wote watafanyiwa hesabu na kila mmoja atalipwa kwa yale aliyoyatenda. Yule aliyefanya mazuri, atalipwa mazuri, na yule aliyefanya maovu, atalipwa maovu. Kuamini pia kwamba Pepo ni nyumba ya watiifu na kwamba Moto ni adhabu kwa wale wenye kuasi.

Kadhalika inatakiwa kuamini uwepo wa Malaika na aina zao mbalimbali. Vilevile kuamini Vitabu vilivyoteremshwa na kutumilizwa kwa Mitume. Inatakiwa kuwaamini wale waliotajwa ndani ya Qur-aan. Kuhusu wale ambao hawakutajwa ndani yake, tunaamini kuwa Allaah ana Mitume tusiowajua. Vilevile Yeye (Subhaanah) ana Vitabu tusivyovijua. Kama tulivyotangulia kusema tunaamini kufufuliwa baada ya kufa kwa njia iliyofafanuliwa.

Vilevile tunaamini Qadar, kheri na shari, ni yenye kutoka kwa Allaah (Ta´ala). Kuhusiana na hilo tunaamini pia kwamba Allaah ni mwadilifu na hamnyanyasi wala kumdhulumu yeyote. Hamwadhibu yeyote isipokuwa kwa dhambi zake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ

“Hakika Allaah hadhulumu uzito wa atomu.”[2]

وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

“Mola wako si Mwenye kudhulumu waja.”[3]

Hizi ndio nguzo za imani sita. Zote ni imani zilizofungamana na moyo na kuzitendea kazi ni jambo linakwenda sambamba na imani.

[1] Muslim (01).

[2] 04:40

[3] 41:46

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 21-24
  • Imechapishwa: 21/09/2021