16. Jambo la tatu mfungaji anatakiwa kulipatiliza

3 – Miongoni mwa mambo muhimu ambayo tunatakiwa kuyapatiliza katika mwezi wa Ramadhaan ni kutafuta kutoka na kupitia mwezi huo kumcha Allaah (Jalla wa ´Alaa). Haya ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ambalo funga imewekwa katika Shari´ah kwa ajili yake. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

يأيها الذينءامنوا كتب عليكم الصيام كما كتب على الذين من قبلكم لعلكم تتقون

 “Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[1]

Kwa swawm na kwa kutekeleza ´ibaadah hii muislamu anapita njia kuu na yenye kubarikiwa inayompelekea katika kumcha Allaah (Jalla wa ´Alaa). Swawm ni fursa kwako ya kujifanyia akiba ya kumcha Allaah na ya kuwa miongoni mwa wenye kumcha Allaah.

Kumcha Allaah ni kule kutenda kwa kumtii Allaah, juu ya nuru itokayo kwa Allaah hali ya kutaraji thawabu za Allaah. Sambamba na hilo uache maasi ya Allaah, juu ya nuru itokayo kwa Allaah hali ya kuogopa adhabu ya Allaah.

Hebu wacha tusimame kidogo tuzingatie ni namna gani swawm inahakikisha kumcha Allaah na kupitia swawm inamfanya mtu kuwa na akiba ya uchaji? Muislamu mwaka mzima amezowea wakati wa mchana mambo aliyoyazowea kama vile kula chakula asubuhi, amezowea kula chakula cha jioni, amezowea kunywa aina mbalimbali ya kinywaji. Lakini mambo haya aliyoyazowea anakuwa ni mwenye kuviacha mara moja pale tu unapoingia mwezi wa Ramadhaan licha ya kuwa ameyazowea. Lakini anayaacha na kuyaepuka kikamilifu. Hafanyi hivo kwa sababu nyingine isipokuwa ili kupata thawabu za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Huku ndio kumcha Allaah. Utamuona mfungaji anajizuilia na chakula na kinywaji vilivyoko mbele yake hata kama atakuwa peke yake na hakuna mtu yeyote anayemuona. Anafanya yote hayo kwa ajili ya kumtii Allaah (Ta´ala). Haya yanayomtokea muislamu mchana wa Ramadhaan anatakiwa kuyaendeleza katika maisha yake yote juu ya kila utiifu aliyoamrisha Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na juu ya kila jambo alilomkataza Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Wewe ambaye umejizuilia mchana wa Ramadhaan kutokamana na chakula na kinywaji, kwa ajili ya kumtii Allaah, basi inakupasa kujizuilia kutokamana na kila jambo ambalo Allaah amekuharamishia katika kila wakati na kila kipindi. Mola wa Ramadhaan ndio Mola wa miezi yote (Subhaanahu wa Ta´ala). Yule ambaye ni lazima kumtii katika Ramadhaan analazimika kutiiwa katika vipindi vyote. Ikiwa umeimiliki nafsi yako na ukaizuilia kutokamana na kumuasi Yeye (Ta´ala) na pia ukayaepuka yale mambo uliyoyazowea, kwa ajili ya kumtii Allaah (Jalla wa ´Alaa) mchana wa Ramadhaan, basi inakupasa kuizoweza nafsi yako kuyatekeleza mambo haya katika kila wakati na kila kipindi.

Kukiepuka chakula, kinywaji na vifunguzi vyengine wakati wake ni katika Ramadhaan. Nakusudia ulazima wa kufanya hivo. Hayo yanafanyika kuanzia kupambazuka kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua. Lakini kufunga na kujizuilia na vitu vya haramu wakati wake ni katika maisha mazima. Ni lazima kupambana na nafsi yako mapambano kamilifu juu ya kujizuilia na kila jambo ambalo Allaah amekuharamishia. Ukichupa mpaka, ukavuka mpaka au ukatumbukia ndani ya jambo la kimapungufu basi unatakiwa kuiridiki nafsi yako kwa tawbah, kujutia na kurejea kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

[1] 01:183

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 17/04/2022