3 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila kitendo cha mwanadamu kinalipwa maradufu tendo jema moja mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Mfungaji ana furaha mbili: furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola wake. Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Katika Hadiyth kuna dalili juu ya ubora wa funga na nafasi yake ya juu mbele ya Allaah (Ta´ala). Katika Hadiyth hii kumetajwa fadhilah zake kuu nne:

1 – Wafungai watalipwa ujira wao pasi na hesabu. Matendo hulipwa mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Isipokuwa tu swawm. Kuongezwa kwake hakufupiki katika idadi hii. Bali Allaah (´Azza wa Jall) huizidisha mara nyingi. Kwa sababu swawm ni katika subira. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika si venginevyo wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[2]

al-Awzaa´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Haipimwi kwenye kipimo. Bali huzidishwa mara nyingi.”[3]

 2 – Allaah (Ta´ala) ameiegemeza swawm Kwake miongoni mwa matendo mengi. Hili – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwa sababu inachukua nafasi ya mchana wake mzima. Mfungaji hujikuta ameyaacha matamanio yake ilihali anayatamani. Hilo khaswa katika kipindi cha majira ya moto kutokana na ukali wa joto. Jengine ni kwa sababu funga ni siri kati ya mja na Mola Wake na hakuna anayejua hali yake isipokuwa Allaah (Ta´ala) pekee. Kwa hivyo ni kitendo kilichojificha ambacho viumbe hawakioni wala hakiingiliwi na jambo la kujionyesha.

3 – Mfungaji atafurahi pindi atapokutana na Mola Wake. Hayo ni kutokana na yale malipo na thawabu atazoziona na amepangiwa malipo juu yake kwa kuikubali swawm ambayo Allaah amemjaalia.

Kuhusu furaha yake wakati wa kukata kwake swawm ni kwa kule kukamilisha ´ibaadah yake, kusalimika kwake na mambo yanayoiharibu na kupata yale aliyokuwa amekatazwa ambayo yanaafikiana na maumbile yake. Furaha hii ni yenye kusifiwa kwa sababu ni kufurahikia kumtii Allaah na kukamilisha swawm iliyoahidiwa ujira mkubwa.

4 – Harufu itokayo mdomoni mwa mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski, jambo ambalo litakuwa siku ya Qiyaamah. Ndio kipindi ambacho kutadhihiri malipo ya matendo. Kutokana na upokezi unaosema:

“Ni nzuri zaidi mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah.”[4]

Harufu hii, inagwa ni yenye kuchukiza katika pua za watu duniani, lakini ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Kwani imetokana na kumtii Allaah (Ta´ala).

Miongoni mwa fadhilah za funga ni kwamba ni katika sababu za kusamehewa madhambi na kufutiwa maasi. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[5]

Kuna maafikiano juu yake.

Lakini fadhilah hizi anazipata yule ambaye anafunga hali ya kumtakasia nia Allaah kutokamana na chakula, kinywaji na tendo la ndoa. Aidha akavizuilia viungo vyake vya mwili kutokamana na madhambi. Hii ndio swawm iliyowekwa katika Shari´ah ambayo imepangiliwa thawabu kuu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[6]

Ee Allaah! Tuhifadhie swawm zetu, uifanye kuwa mwombezi wetu, tusaidie kupitia funga juu ya kukutii, tuepushe na njia za kukuasi na utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151) na (164) na tamko ni lake.

[2] 39:10

[3] Tafsiyr Ibn Kathiyr (07/80).

[4] Muslim (1151) na (163).

[5] al-Bukhaariy (38) na Muslim (760). Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… madhambi yake yaliyotangulia.”

udhahiri wake ni kwamba yanasamehewa madhambi makubwa na madogo. Lakini kikosi cha wanazuoni wengi wanaona kuwa makusudio na madhambi madogo.

[6] al-Bukhaariy (6057). Tazama maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah juu ya maana yake katika “Minhaaj-us-Sunnah” (05/197-198).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 17/04/2022