4 –  Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Unapoingia mwezi wa Ramadhaan basi milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hutiwa pingu.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Imekuja katika upokezi wa Muslim:

“Hufunguliwa milango ya rehema.”[1]

Hadiyth hii ni dalili kuhusu ubora wa mwezi wa Ramadhaan na utukufu wa sifa zake za kipekee. Allaah ameufadhilisha juu ya miezi mingine na akautofautisha kwa mambo yasiyopatikana katika miezi mingine miongoni mwa mambo yatayomvutia mtu katika matendo mema, wema na ihsaan.

Katika mwezi huu mtukufu inafunguliwa milango ya Pepo na inafungwa milango ya Moto. Hayo – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kutokana na zile kheri nyingi zinazopatikana ndani ya Ramadhaan na kuongezeka watu kuzielekea zile sababu za msamaha na radhi za Allaah. Matokeo yake shari inapungua ulimwenguni kwa sababu wanafungwa minyororo na pingu wale mashaytwaan waovu ili wasiwashughulishe waislamu funga, kisomo cha Qur-aan na kumtaja Allaah (Ta´ala) na kila kitendo miongoni mwa vitendo vyema na kila neno miongoni mwa maneno yenye kheri. Hapa tunapata siri juu ya kujirejea wengi katika watenda maasi, kutubu kwao kwa Allaah, kupupia kwao matendo mema na kuhudhuria kwao misikiti katika mwezi huu mtukufu. Shaytwaan aliyefungwa minyororo wanaweza kufungwa kusumbua. Lakini haya yanakuwa kwa uchache na kidogo ukilinganisha na inavokuwa miezi mingine. Na hilo linakuwa kwa kiasi cha ukamilifu na upungufu wa swawm. Yule ambaye swawm yake ni kamilifu kwa njia ya kwamba amehifadhi sharti na zile adabu za funga, basi humzuia shaytwaan kikweli na hivoy funga yake isiingiliwe na upungufu. Hata hivyo kitendo cha wao kufungwa haina maana kwamba hakuwezi kutokea shari wala maasi kabisa. Kwa sababu zipo sababu nyenginezo mbali na shaytwaan kama mfano wa nafsi mbaya, tabia mbaya na mashaytwaan wa kiwatu. Vilevile kuna uwezekano makusudio ya wanaofungwa minyororo ni:

“… wale mashaytwaan waovu.”

Kama ilivyopokelewa katika baadhi ya mapokezi[2]. Kwa hivyo taathira inabaki kwa wale wasiokuwa waovu. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ni lazima kwa waislamu kuharakia kutenda matendo mema na aina mbalimbali ya utiifu. Awe ni mwenye kupanga wakati wake na mwenye kufaidika na misimu ya utiifu. Analazimika kuchukua tahadhari kubwa ya kukesha nyusiku za Ramadhaan ili apate uchangamfu wakati wa mchana. Ikiwa imekatazwa kukesha nje ya Ramadhaan basi ndani ya Ramadhaan inakuwa kubaya zaidi na khaswa kukesha juu ya vyombo vya upuuzi na pumbao au katika vikao vitupu ambavyo madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Kubwa zaidi kuliko hayo ni kulala sehemu kubwa ya mchana. Bali pengine hata mtu akakosa zile swalah zilizofaradhishwa.

Ee Allaah! Tuamshe kutoka katika usingizi wa ughafilikaji, tuwafikishe kuweza kujiandaa kabla ya kuondoka, tupe ilhamu ya kuvuna zama wakati wa muhula na tusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1899) na Muslim (1079).

[2] Sunan an-Nasaa´iy (04/129).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 17/04/2022