07. Hadiyth ”Inapoingia Ramadhaan basi milango ya Pepo hufunguliwa… “

998- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Inapoingia Ramadhaan basi milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hutiwa pingu.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Katika upokezi wa Muslim imekuja:

”Inapoingia Ramadhaan basi milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo.”

Ameipokea at-Tirmidhiy, Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” na al-Bayhaqiy kutoka kwa Abu Bakr bin ´Ayyaash, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah kwa tamko lisemalo:

“Usiku wa kwanza  wa Ramadhaan mashaytwaan na wale majini waovu hutiwa pingu, milango ya Moto hufungwa ambapo hakufunguliwi mlango wowote na milango ya Pepo hufunguliwa ambapo hakufungwi mlango wowote. Ananadi Mwenye kunadi: “Ee mwenye kutaka kheri! Njoo! Ee mwenye kutaka shari! Koma!” Kuna watu Allaah huwaacha huru na Moto na hilo linakuwa katika kila usiku.”[2]

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni geni.”

an-Nasaa´iy na al-Haakim wamepokea kwa mfano wa muundo huu. al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.”

[1] Swahiyh.

[2] Nzuri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/585)
  • Imechapishwa: 26/05/2018
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy