15. Jambo la pili mfungaji anatakiwa kulipatiliza

2 – Miongoni mwa mambo muhimu, bali ndio muhimu zaidi ambalo mtu anatakiwa kulitilia umuhimu katika swawm yake, ni yeye kuhakikisha maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

Kwa hivyo muislamu anatakiwa kufunga kwa imani na kwa matarajio. Asifunge kidesturi. Kwa msemo mwingine ni kwamba asifunge kwa sababu familia, ndugu na marafiki zake wamefunga na yeye ndio maana akafunga. Wala asifunge kwa sababu ya kuepukwa kusemwa na akaambiwa kuwa ni mwenye kula. Wala asifunge kwa sababu ya kuwaonyesha watu, kupenda asifiwe na kutapwa. Hafungi kutokana na chochote katika malengo haya. Si venginevyo anafunga kwa imani na matarajio. Anafunga kwa kumwamini Allaah, ahadi ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kwa wafungaji na kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) atawapa malipo yao pasi na hesabu. Anafunga hali ya kuamini kuwa Allaah (Ta´ala) amefaradhisha funga juu ya waja Wake.

 Vivyo hivyo anafunga kwa matarajio kwa njia ya kwamba anatarajia kutokana na swawm yake, utekelezaji wake wa kumtii Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) katika mwezi huu mtukufu ujira na thawabu mbele ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Wafungaji wana ujira mkuu na thawabu tukufu mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Imepokelewa katika Hadiyth-ul-Qudsiy kuwa Allaah anasema:

“Swawm ni Yangu na mimi ndiye Nitailipa.”[2]

Haya yanabainisha ukubwa wa thawabu na ujira kwa wafungaji mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Muislamu anatakiwa kuichunga swawm yake uchungaji mkubwa. Imepokelewa katika Hadiyth nyingine ambapo amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mfungaji ana furaha mbili; furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm yake na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola Wake.”[3]

Mfungaji atafurahi furaha kubwa wakati atapokutana na Allaah (Jalla wa ´Aaa) siku ya Qiyaamah. Kwani Allaah amewaandalia wafungaji ujira mkuu na thawabu tukufu. Bali Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amewafanyia wafungaji mlango maalum ambapo wataingia kupitia mlango huo kuelekea ndani ya Pepo. Mlango huo unaitwa “ar-Rayaan”[4]. Hayo yamethibiti kutoka katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hivyo muislamu anapaswa kupatiliza jambo hili kuanzia mwanzoni mwa mwezi mpaka mwishoni mwake; afunge kwa imani na kwa matarajio. Afunge hali ya kumwamini Allaah na kwamba Yeye (Subhaanah) ametuwajibishia swawm na hali ya kutaraji kupata thawabu na ujira kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

[1] al-Bukhaariy (37, 1875) na Muslim (1268) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] al-Bukhaariy (1761) na Muslim (1151) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] al-Bukhaariy (1771) na Muslim (1945) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] al-Bukhaariy (1896, 3257) na Muslim (1152) kupitia kwa Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 17/04/2022