14. Jambo la kwanza mfungaji anatakiwa kulipatiliza

1 – Miongoni mwa mambo muhimu ambayo tunapaswa kuyapatiliza katika mwezi wa Ramadhaan ni kuhifadhi swawm ambayo ndio faradhi ya mwezi huu.

Watu inapokuja katika swawm wanatofautiana tofauti kubwa. Hawako katika ngazi moja ijapo wote ni wenye kushirikiana katika kujizuilia kutokamana na chakula, kinywaji na vifunguzi vengine kuanzia pale kunapopambazuka alfajiri mpaka pale jua linapozama. Lakini wanatofautiana katika kuzikamilisha funga zao tofauti kubwa. Aliulizwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wafungaji wepi wenye thawabu nyingi?” Akasema:

“Ni wale wenye kumtaja Allaah kwa wingi.”[1]

 Ni jambo linalotambulika ya kwamba wafungaji wanatofautiana tofauti kubwa katika kumwelekea kumtaja Allaah (Ta´ala), Qur-aan na kuhifadhi utiifu.

Wako watu wanaokesha usiku katika kupoteza na kuangamiza wakati, kisha wakiswali Fajr – wakiwa ni miongoni mwa wale wenye kuhifadhi swalah – wanaingia katika usingizi mzito. Huenda baadhi yao wakapitwa na swalah ya Dhuhr na ´Aswr.

Kwa hivyo watu wanatofautiana katika namna ya kufunga tofauti kubwa. Kwa ajili hiyo muislamu anatakiwa kutilia umuhimu kuikamilisha swawm yake, kuijaza utajo wa Allaah, kuelekea kumtii Allaah, kuhifadhi kisomo cha Qur-aan, kuhudhuria vikao vya kheri, kukaa misikitini na apambane na nafsi yake mapambano makubwa.

[1] Ahmad (15614), at-Twabaraaniy katika ”ad-Du´aa” (1887) na katika ”al-Kubraa” (16812).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 17/04/2022