2 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila kitendo cha mwanadamu kinalipwa maradufu tendo jema moja mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Allaah (Ta´ala) amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Mfungaji ana furaha mbili: furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola wake. Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth imefahamisha maana ya swawm wa mujibu wa Shari´ah. Ni kule kujiepusha na chakula, kinywaji na matamanio kwa ajili ya kumwabudu Allaah, kuitikia amri Yake na kukimbilia radhi Zake. Kutokana na maneno yake:

”… kwa ajili yangu.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Anaacha chakula na kinywaji chake kwa ajili yangu.”[2]

Makusudio ya matamanio (الشهوة) ni jimaa. Kuna uwezekano vilevile ikakusanya matamanio yote. Imekuja kwa Ibn Khuzaymah kwa cheni ya wapokezi ambayo ni Swahiyh:

”Anaacha chakula kwa ajili Yangu, anaacha kinywaji kwa ajili Yangu, anaacha ladha yake kwa ajili Yangu na anamwacha mke wake kwa ajili Yangu.”[3]

Qur-aan Tukufu imejulisha kipindi cha swawm katika maneno Yake (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[4]

Allaah akahalalisha kula na kunywa mpaka kupambazuka kwa alfajiri. Kisha akaamrisha kukamilisha swawm mpaka usiku. Hiyo maana yake ni kuacha kula na kunywa katika kitambo hiki. Ni kitambo kati ya kuchomoza kwa alfajiri mpaka usiku.

Makusudio ya kula na kunywa kukifikisha chakula au kinywaji kupitia njia ya mdomo au ya pua pasi na kuja ni aina gani ya kilicholiwa au kilichonywewa.

Kuhusu sindano za kimatibabu anazodungwa mgonjwa kwa njia ya mishipa au misuli – zinaweza kuwa kwa ajili ya dawa au kwa ajili ya lishe – ni suala ambalo wanazuoni wametofautiana. Miongoni mwao wako ambao wanaona kuwa zinafunguza kwa njia yoyote na wako wengine ambao wanapambanua[5]. Endapo mfungaji atazichelewesha mpaka wakati wa usiku ndio salama zaidi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Kiache kile chenye kukutia shaka na badala yake kiendee kile kisichokutia shaka.”[6]

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hivyo basi, yeyote atakayejiepusha yenye kutia shaka, basi atakuwa amejiepushia shaka katika dini yake na heshima yake.”[7]

Ambaye atahitajia kitu katika mambo hayo basi mara nyingi ni kwamba ni mgonjwa na hivyo inaruhusiwa kwake kuacha kufunga.

Kuhusu sindano za kimatibabu za kawaida udhahiri ni kwamba hazifunguzi. Kwa sababu hazilishi. Bali zinaondosha kile kilichomo tumboni.

Mfungaji hafungui kwa kutumia dawa ya pumu na sprei za pumzi. Kwa sababu hazifiki tumboni. Bali zinaenda katika mapafu kupitia njia ya trachea. Kwa hivyo sio kula wala kunywa. Endapo kutakadiriwa kwamba kuna kitu kinafika tumboni basi ni kidogo chenye kutiliwa shaka. Kukilinganisha na usukutuaji na Siwaak ni kipimo cha wazi[8].

Wala mtu hafungui kwa kutia wanja na dawa ya tone machoni. Ni mamoja mtu atahisi ladha yake kooni au hatohisi.

Kuhusu tone puani linafunguza likifika tumboni au kooni. Kwa sababu pua ni njia inayofika tumboni. Isitoshe kutokana na Hadiyth ya Luqaytw bin Swabirah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kishindo katika kupalizia isipokuwa kama utakuwa umefunga.”[9]

Ee Allaah! Tupe ufahamu katika dini yetu, uturuzuku kuweza kuitendea kazi, kunyooka juu yake na tuwepesishie mepesi na tuepushe na magumu, utusamehe Aakhirah na duniani na wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151) na (164) na tamko ni lake.

[2] Fath-ul-Baariy (04/103).

[3] Swahiyh Ibn Khuzaymah (03/197). Tazama ”Fath-ul-Baariy” (04/107).

[4] 02:187

[5] Tazama ”Fataawaa al-Muta´aliqatu bit-Twibbi wa Ahkaam-il-Mardhwaa”, uk. 107 na ”Ahkaam-Haqn at-Twabiyyah”.

[6] at-Tirmidhiy (2518), an-Nasaa´iy (08/327) na Ahmad (03/249). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh.”

Iko na nyenginezo zinazoitia nguvu kutoka kwa Anas na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum).

[7] al-Bukhaariy (52) na Muslim (1599).

[8] Tazama “Muftwiyraat-us-Swiyaam al-Mu´aaswirah”, uk. 58.

[9] Abu Daawuud (2366), at-Tirmidhiy (788), an-Nasaa´iy (01/66), Ibn Maajah (01/142,153) na wengineo. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 09-11
  • Imechapishwa: 16/04/2022