1 – ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Uislamu umejengeka juu ya vitano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji Nyumba na kufunga Ramadhaan.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Katika Hadiyth hii kuna ulazima wa kufunga swawm ya Ramadhaan na kwamba ni katika nguzo za Uislamu na misingi yake mikubwa. Allaah (Ta´ala) amewafaradhishia waja Wake kutokana na hekima kubwa na siri nyingi ambazo wamezijua baadhi na wengine hawakuzijua.

1 – Miongoni mwa hekima za funga na siri zake ni kwamba ni kumwabudu Allaah ambapo mja anajikurubisha kwa Mola Wake kwa kuyaacha yale mambo anayoyapenda na kuyataka. Anafanya hivo kwa ajili ya kumtii Mola Wake na kutekeleza amri Yake. Hivyo inapata kuonekana ukweli wa imani yake, ukamilifu wa kumwabudu kwake Allaah, nguvu ya kumpenda kwake na kutaraji yale yaliyoko Kwake. Kwa sababu ametambua kuwa radhi za Mola Wake zinapatikana kwa kuyaacha matamanio yake. Kwa hivyo akatanguliza radhi za Mola Wake juu ya matamanio Yake. Kwa ajili hiyo ikawa hali ya waumini wengi endapo watapigwa au wakafungwa kwa ajili ya kula siku moja tu ya Ramadhaan pasi na udhuru wasingefanya hivo.

2 – Miongoni mwa hekima za funga ni kwamba ni sababu ya kumcha Allaah na kuitakasa nafsi kwa kumtii Allaah kwa yale aliyoamrisha na kuyaepuka yale aliyokataza. Amesema (Ta´ala):

يأيها الذينءامنوا كتب عليكم الصيام كما كتب على الذين من قبلكم لعلكم تتقون

 “Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[2]

Uchaji umekusanya kheri zote za duniani na Aakhirah. Kila tunda miongoni mwa matunda ya swawm yanatokamana na kumcha Allaah.

3 – Miongoni mwa hekima za funga ni kuizuilia nafsi kutokamana na matamanio, kuiachisha yale mambo iliyozowea, kuzifanya nyembamba zile njia za mishipa za mja kwa kuzuia chakula na kinywaji. Matokeo yake unadhoofika ushawishi wa shaytwaan na madhambi yanapungua.

4 – Miongoni mwa hekima za funga ni kwamba moyo unakuwa msafi na unaacha mambo ya fikira. Kwa sababu kufanya yale mambo ya matamanio kunaufanya moyo kuwa msusuwavu na kupofusha haki ilihali swawm inahifadhi uzima na nguvu ya moyo na viungo vya mwili.

5 – Miongoni mwa hekima za funga ni kutambua neema za Allaah kwa kushiba na hali nzuri pale anapokumbuka kwa funga wale wenye njaa katika mafukara na masikini. Matokeo yake akamshukuru Mola Wake na akahisi machungu ya wale ndugu zake masikini. Neema mtu hahisi thamani yake isipokuwa pale anapozikosa.

6 –  Miongoni mwa hekima za funga ni zile faida za kiafya inazopelekea kwa kupunguza chakula na kuhifadhi afya ya mwili kwa kupanga nyakati za chakula na kupumzisha mfumo wa tumbo kwa kipindi fulani.

Kwa mukhtaswari ni kwamba hekima za funga ni kuu na faida zake ni nyingi. Allaah ameipangia malipo na ujira mkubwa kiasi cha kwamba endapo atayafikiria ambaye amefunga basi angelifurahi sana na kutamani mwaka mzima uwe Ramadhaan.

Ee Allaah tuwafikishe kufuata uongofu, tuepushe sababu za maangamivu, turuzuku uelewa katika dini na utekelezaji kwa mujibu wa Sunnah za Nabii wa mwisho na utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote.

[1] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[2] 02:183

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 07-08
  • Imechapishwa: 16/04/2022