16. Ibn ´Abbaas aliona mikono ya Maswahabah wa kike

6 – Imesihi kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh):

”Ulishuhudia ´iyd pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: ”Ndio, kama isingelikuwa kwa sababu ya udogo wangu basi nisingelishuhudia. Alipofika kwenye bendera karibu na nyumba ya Kathiyr bin as-Swalt aliswali. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashuka chini[1]. Nilimuona akiwaonyesha wanamme wakae chini kisha akawageukia. Halafu akawaendea wanawake akiwa pamoja na Bilaal na akasoma:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا جَاءَكَ الْمُؤْمِنَاتُ يُبَايِعْنَكَ عَلَىٰ أَن لَّا يُشْرِكْنَ بِاللَّـهِ شَيْئًا

”Ee Nabii! Wakikujia waumini wa kike kuahidiana nawe ahadi ya utiifu kwamba hawatomshirikisha Allaah na chochote… ”[2]

Wakati alipomaliza kuisoma akasema: ”Je, nyinyi mko hivo?” Mwanamke mmoja akasema: ”Ndio, ee Nabii wa Allaah.” Akawawaidhi, akawakumbusha na akawaamrisha kutoa swadaqah. Bilaal akatandaza nguo yake na kusema: ”Haya! Nawatoa fidia wazazi wangu kwenu!” Nikawaona wanaanza kuchimba kwa mikono yao na kutupa cheni za miguuni na pete kwenye nguo ya Bilaal. Halafu yeye na Bilaal wakaondoka nyumbani kwake.”[3]

[1] Hapa kuna ishara ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alihutubia juu ya kitu kilichoinuka, pengine ilikuwa juu ya kipando cha mnyama. Sikutaja juu ya mimbari kwa sababu wanazuoni hawatambui kuwa alihutubia juu ya mimbari siku ya ´iyd, kama walivyothibitisha hilo Ibn-ul-Qayyim, Ibn Hajar na wengineo. Siku ya ´iyd alikuwa akihutubia kwa kusimama juu ya mimbari yake, kama inavyotambulika kwa Jaabir:

”Kisha akasimama hali ya kumwegemea Bilaal… ”

Ibn-ul-Qayyim amesema:

”Hakukuwepo na mimbari ya kupanda. Wala mimbari ya Madiynah haikuwa inatolewa nje. Hakika mambo yalivyo ni kwamba alikuwa akihutubia hali ya kusimama kwenye ardhi.” (Zaad-ul-Ma´aad (1/445))

Halafu akataja Hadiyth ya Jaabir, Hadiyth ya Ibn ´Abbaas na Hadiyth nyingine yenye kuitia nguvu kutoka kwa Jaabir kisha akasema:

”Hapa inafahamisha kuwa alikuwa akihutubu juu ya mimbari au juu ya kipando chake cha mnyama. Pengine alikuwa amejengewa mimbari ya matofali, udongo au kitu kingine.

Imesemekana kuwa hapana shaka yoyote juu ya usahihi wa Hadiyth hizi mbili na wala hapana shaka yoyote ya kwamba mimbari yake haikuwa inatolewa nje ya msikiti. Mtu wa kwanza kuitoa nje alikuwa ni Marwaan bin al-Hakam ambapo akasimangwa. Kuhusu mimbari ya matofali na udongo, al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba mtu wa kwanza kuijenga alikuwa ni Kathiyr bin as-Swalt katika uongozi wa Marwan huko Madiynah. Pengine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama mahali palipoinuka au benchi. Baada ya hapo anaondoka kwenda kwa wanawake na kuwahutubia, kuwawaidhi na kuwakumbusha – na Allaah ndiye anajua zaidi.” (Zaad-ul-Ma´aad (1/447))

[2] 60:12

[3] al-Bukhaariy (2/273), kupitia kwake Ibn Hazm (3/217), Abu Daawuud (1/174), kupitia kwake al-Bayhaqiy (3/307), an-Nasaa’iy (1/277), Ahmad (1/331) na ziada ni yake, Ibn-ul-Jaaruud katika ”al-Muntaqaa” (263) na Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” (2/356/1458). Baada ya Ibn Hazm kujengea hoja kwamba uso wa mwanamke sio uchi akasema:

”Ibn ´Abbaas, ambaye alikuwa ameshuhudia na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aliona mikono ya wanawake. Kwa hivyo kuna dalili ya wazi juu ya kwamba mikono na nyuso za wanawake sio uchi. Vinginevyo ingelazimika kuifunika.”

Kutokana na kwamba Hadiyth inataja jinsi wanawake walivyokula kiapo cha utii kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni dhahiri kuwa ilitokea baada ya Aayah ya kuteremshwa Aayah ya jilbaab, ambayo iliteremshwa mwaka wa 03. Aayah ya kula kiapo cha utii iliteremshwa mwaka wa 06. Kwa mujibu wa ”Fath-ul-Baariy” (02/377) Ibn ´Abbaas alishuhudia tukio hilo baada ya kufunguliwa Makkah, jambo ambalo linatia nguvu hoja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 67-69
  • Imechapishwa: 10/09/2023