15. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan I

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Na Yeye (Subhaanah) kwa yale aliyojisifia na kujiita kwayo Nafsi Yake, kajumuisha baina ya ukanushaji na uthibitisho. Hivyo hakuna upotofu wowote kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa yale waliyokuja nayo Mitume, kwani hakika ni Njia iliyonyooka; Njia ambayo Kawaneemesha Kwayo waifuatayo, miongoni mwa Manabii, wakweli, mashahidi na waja wema.

Kunaingia katika haya yale aliyojisifia Allaah Nafsi Yake Mwenyewe katika Suurah “al-Ikhlaasw”, ambayo ni sawa na theluthi ya Qur-aan, ambapo Kasema:

 

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja Pekee. Allaah ambaye ni Mwenye kukusudiwa. Hakuzaa na wala Hakuzaliwa. Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.”(112:01-04)

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

”Allaah, hakuna mungu wa haki ila Yeye – Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu. Haumchukuwi usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai [anayeombea] mbele Yake bila ya idhini Yake. Anajua yaliyo mbele yao [viumbe] na yaliyo nyuma yao. Wala hawakizunguki chochote kile katika Elimu Yake isipokuwa kwa Alitakalo. Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye mkuu.”(02:255)

MAELEZO

Na Yeye (Subhaanah) kwa yale aliyojisifia na kujiita kwayo Nafsi Yake… – Bi maana katika Aayah na Hadiyth nyingi. Ukanushaji umekuja kwa njia ya ujumla na uthibitisho umekuja kwa njia ya upambanuzi. Huu ndio mfumo wa Qur-aan na Sunnah ambapo ukanushaji unakuwa kijumla:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.” (42:11)

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye [washirika] na hali ya kuwa nyinyi mnajua [kuwa hana].” (02:22)

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua [mwengine] mwenye Jina kama Lake?” (19:65)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)

Kuna Aayah nyenginezo nyingi.

Uthibitisho unakuwa kwa njia ya upambanuzi:

وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Naye ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hikmah.” (14:04)

لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (02:143)

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ

“Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja Pekee. Allaah ni Mwenye kukusudiwa”.” (112:01-02)

غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (02:218)

هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ

“Yeye Ndiye ndiye Mfalme, Mtakatifu, Mwenye amani.” (59:23)

Kuna Aayah nyenginezo zilizofafanuliwa kuhusu sifa na majina Yake (Subhnaanahu wa Ta´ala).

Katika Aayah za Qur-aan na Sunnah amekusanya kati ya ukanushaji na uthibitisho. Ukanushaji unakuwa kwa njia ya ujumla ambapo ndani yake unamtakasa Allaah na yale yote ambayo hayalingani Naye na kumtakasa (Subhaanahu wa Ta´ala) kutokana na yale wanayosema maadui wa Mitume (´alayhimus-Salaam). Sambamba na hilo ndani yake kunakuwa kuthibitisha majina na sifa Zake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia ya upambanuzi.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com