15. Sababu ya kumi na moja ya talaka ambayo ni kukanusha wema wa mwanandoa mwenza

11 – Kukanusha neema na wema

Ni mamoja mkanushaji ni mume au mke. Hadiyth imetaja kwamba mara nyingi wanaofanya hivo ni wanawake. Kama alivyosimulia Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea Khutbah ambapo akasema: ”Toeni swadaqah kwa wingi, enyi wanawake. Kwani hakika nyinyi ndio wakazi wengi wa Motoni siku ya Qiyaamah.” Akasimama mwanamke mmoja asiyekuwa katika wale wanawake wenye vyeo vya juu na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah, ni kwa nini sisi ndio wakazi wengi wa Motoni?” Akasema: ”Mnakithirisha  laana na mnakufuru wema.”[1]

Maana yake ni kwamba anakanusha neema ya mume kwa sababu ya hali ambayo haikumpendeza. Utamsikia mwanamke anamwambia mume maneno kama ´sijawahi kuona kutoka kwako chochote, wewe hujanifanyia chochote, wewe hujanifanyia na wala sina haja`. Huku ni kukufuru neema. Mfano wa hali kama hizi mume huingiwa na kiburi katika nafsi yake na khaswa pale ambapo yatakithiri kwa mwanamke na yeye anamkanusha na kumwomba mume wake talaka.

Kuna uwezekano vilevile mume anapoingia na anapotoka anakanusha juhudi za mke wake, yale anayoyafanya nyumbani, anayomfanyia wakati wa kukutana naye, anayoyafanya wakati anaposafisha na kuipangilia nyumba yake. Anajifanya hayajui yote haya na kuyakanusha. Hayo yanafanywa mara kwa mara na hivyo mambo yanabadilika. Hatimaye ikampelekea mwanamke kuzembea na pengine mambo yakaenda mbali zaidi ikamfanya mwanamke asimfanyie wajibu wake mume wake. Hapo ndipo matatizo huanza na vifua vikaingiwa na dhiki na wanakuwa hawaoni jengine zaidi ya talaka.

[1] al-Bukhaariy (304) na Muslim (79).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 08/04/2024