Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

3 – Mwenye kumtii Mtume na akampwekesha Allaah Mmoja, basi haijuzu kwake kufanya urafiki na wale wanaompinga Allaah na Mtume Wake, hata kama itakuwa ni jamaa wa karibu. 

MAELEZO

Ubainifu wa suala la tatu. Bi maana mwenye kumtii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akatekeleza maamrisho yake, akajiepusha na makatazo yake, akasadikisha maelezo Yake, akampwekesha Allaah na akamtakasia ´ibaadah Yeye pekee na ´ibaadah hiyo ikaafikiana na Shari´ah ya Allaah, akasubiri ahadi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haijuzu kwake kujenga urafiki na wale wanaompinga Allaah na Mtume Wake. Kujenga urafiki (الموالاة) maana yake ni kuwapenda. Anayempinga Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yule ambaye anamuasi Allaah na Mtume Wake na anayefarikiana na dini Yake; naye ni kafiri. Haijuzu kujenga urafiki wala kumpenda kafiri. Huu ni mmoja wa misingi ya dini; msingi wa kupenda na kuchukia. Muislamu mpwekeshaji hampendi kafiri na wala hajengi naye urafiki. Bali anamchukia hata akiwa ni jamaa wa karibu. Haijalishi kitu hata akiwa ni baba yake, mama yake na ndugu yake wa nasaba anatakiwa kumchukia kwa ajili ya dini na wala asimpendi. Anatakiwa kumzingatia kuwa ni adui yake. Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ

“Enyi mlioamini! Msimchukue adui Wangu na adui wenu kuwa marafiki.”[1]

al-Baghawiy amesema:

“Ameeleza kuwa imani ya waumini inaharibika kwa kuwapenda makafiri na kwamba ambaye ni mumini hampendi ambaye amekufuru ijapo atakuwa ni katika jamaa zake.”[2]

[1] 60:01

[2] Tafsiyr-ul-Baghawiy (05/50).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 31
  • Imechapishwa: 04/02/2023