Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

2 – Hakika Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake; si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

MAELEZO

Ubainifu wa suala la pili ni kwamba tunatakiwa kutambua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko na haki na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Usichanganye kati ya haki hizo mbili. Allaah haki Yake ni kuabudiwa Yeye pekee. ´Ibaadah haisihi isipokuwa kwa kumtakasia nia Allaah na kumfuata Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Ibaadah haisihi isipokuwa kwa sharti hizi mbili:

1 – Kumtakasia nia Allaah.

2 – Kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah.”[2]

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[3]

´Ibaadah ni yale maamrisho na makatazo. Utambulisho wake ni jina lililokusanya yale yote anayoyapenda Allaah na kuyaridhia katika maneno, matendo yaliyojificha na yaliyo wazi[4].

´Ibaadah ni kile kilele mwisho cha maadhimisho. Kwa hiyo si haki isipokuwa ya Yule ambaye ana kilele cha mwisho cha neema; ambaye ni Muumbaji, Mruzukaji, Mwenye kuhuisha, Mwenye kufisha, Mwenye kulipa thawabu na Mwenye kuadhibiwa. Yeye ndiye Mwenye msingi wa neema na matawi yake. Utapomwelekea mwingine – Ametakasika pakubwa sifa hii iwe ya mwingine – itakuwa si vyengine isipokuwa ni dhuluma, uadui, kufuru, ukanushaji na utakuwa umetoka katika nuru sahihi na umeingia ndani ya giza lenye madhara. Ni ipi dhana yako kwa ambaye amemwelekezea ´ibaadah yake kitu kisichokuwa na uhao, kisichokuwa na hisia wala hisia?[5]

Swalah ni miongoni mwa ´ibaadah na hivyo ni haki ya Allaah pekee. Haridhii mtu aswali kwa ajili ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Jibriyl au mwezi. Vivyo hivyo swawm na hajj. Haitakiwi kwa mtu kufunga wala kuhiji kwa ajili ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kadhalika du´aa haridhii amuombe yeye na wakati huohuo ukamuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haridhii umchinjie Yeye kisha umchinjie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haridhii umtegemee Yeye kisha umtegemee Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”

Ni yenye kuenea. Kila asiyekuwa Allaah ni yeyote. Kwa maana nyingine usimuomba Malaika, Mtume, Nabii, mtu, jiwe, jini, kitu kisichokuwa na uhai wala vyenginevyo. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَجَعَلُوا لِلَّـهِ مِمَّا ذَرَأَ مِنَ الْحَرْثِ وَالْأَنْعَامِ نَصِيبًا فَقَالُوا هَـٰذَا لِلَّـهِ بِزَعْمِهِمْ وَهَـٰذَا لِشُرَكَائِنَا ۖ فَمَا كَانَ لِشُرَكَائِهِمْ فَلَا يَصِلُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَا كَانَ لِلَّـهِ فَهُوَ يَصِلُ إِلَىٰ شُرَكَائِهِمْ ۗ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ 

“Wamemfanyia Allaah fungu katika mimea na wanyama Aliyoumba wakasema: “Hili ni la Allaah – kwa madai yao – na hili ni kwa ajili ya washirika wetu. Basi yaliyokuwa kwa ajili ya washirika wao hayamfikii Allaah na yaliyokuwa kwa ajili ya Allaah hufika kwa washirika wao. Uovu ulioje wanayoyahukumu!”[6]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema: “Hakika Mimi ni Mwenye kujitosheleza kutohitajia washirika. Hivyo basi yule atakayefanya kitendo akanishirikisha Mimi pamoja na mwingine, basi nitamwacha yeye na shirki yake.”[7]

[1] 72:18

[2] 03:31

[3] 18:110

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/149).

[5] Tafsiyr Imaam-ish-Shaafi´iy (03/1461), Majmuu-ul-Fataawaa (28/152) ya Ibn Taymiyyah na ”Tafsiyr” (01/203) ya Ibn Kathiyr.

[6] 06:136

[7] Muslim (2985).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 03/02/2023