Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1 – Allaah ametuumba, akaturuzuku na hakutuacha bure tu bila ya malengo. Bali amewatumia Mtume; mwenye kumtii, ataingia Peponi, na yule mwenye kumuasi, ataingia Motoni. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, tukamuadhibu adhabu kali sana.”[1]

MAELEZO

Ubainifu wa suala la kwanza:

“Utambue kuwa Allaah ametuumba, akaturuzuku na hakutuacha bure tu bila ya malengo. Bali amewatumia Mtume.”

Mtume huyu amekuja akiwa na maamrisho na makatazo. Aidha Allaah akamteremshia Qur-aan na akampa Sunnah ambayo ni Wahy wa pili. Yule mwenye kumtii Mtume huyu hali ya kutekeleza maamrisho ataingia Peponi, na yule mwenye kumuasi ataingia Motoni. Ni lazima ujue kuwa umeumbwa kwa lengo hili. Hukuumbwa kama wanyama kwa ajili ya kula na kunywa. Bali umeumbwa ili ufanye matendo.

Maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, tukamuadhibu adhabu kali sana.”

Hapa wanazumgumzishwa ummah huu wa Muhammad kuwa wametumiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Fir´awn alitumiwa Mtume, ambaye ni Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini akamuasi. Ndipo Allaah akamuadhibu kwa mali yake adhabu kali. Allaah alimwangamiza yeye na wafuasi wake na akawazamisha. Miili yao ikazamishwa na roho zao zikatiwa Motoni na kuchomwa.

Katika Aayah hii kuna dalili ya kwamba yule asiyemtii Mtume basi Allaah atamuadhibu, kama ambavyo Allaah alimuadhibu Fir´awn.

[1] 73:15-16

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 03/02/2023