12. Dalili ya kutanguliza elimu mbele kabla ya kuzungumza na kutenda

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[1]

Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

Tambua – Allaah akurehemu – kwamba ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke, kujifunza masuala haya matatu na kuyatendea kazi:

MAELEZO

Hapa kuna dalili ya elimu na matendo ambayo imamu ameyaashiria pale aliposema:

”Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

Sufyaan bin ´Uyaynah aliulizwa kuhusu fadhilah za elimu ambapo akajibu:

”Hukusikia maneno Yake pale alipoanza nayo akasema:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah… “

Kisha baada ya hapo akaifuatishia matendo akasema:              

وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“… na omba msamaha kwa dhambi zako.” [2]

Maneno yake mtunzi:

”Tambua – Allaah akurehemu – kwamba ni wajibu… ”

Bi maana ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike kujifunza mambo haya matatu na kuyafanyia kazi. Asipojifunza nayo basi anakuwa ni mtenda dhambi na mwenye kuasi. Kwa sababu kama tulivyotangulia kutaja jambo la lazima ni kile ambacho analipwa thawabu yule mwenye kukifanya na anaadhibiwa mwenye kukiacha. Mfano wa mambo hayo ni swalah; anayeswali Allaah anamlipa thawabu na asiyeswali Allaah anamuadhibu. Vivyo hivyo kuwatendea wema wazazi; yule mwenye kuwatendea wema wazazi Allaah anamlipa thawabu na yule asiyewatendea wema wazazi Allaah anamuadhibu.

Ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike kujifunza mambo haya matatu na kuyafanyia kazi. Yule nwenye kujifunza na baadaye akayafanyia kazi Allaah anamlipa thawabu, na yule asiyejifunza nayo na wala asiyafanyie kazi au akajifunza nayo pasi na kuyafanyia kazi, basi ni mwenye kuadhibiwa na mwenye kupata dhambi. Kwa hivyo kujifunza mambo haya ni faradhi kwa mtu kama ambavyo ilikuwa ni faradhi kujifunza yale mambo manne ya kwanza; kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Uislamu, kutenda kwa mujibu wa Uislamu huo, kulingania kwao na kusubiri juu ya maudhi. Kwa hivyo kujifunza mambo haya ni lazima faradhi na sio jambo la kupendeza tu. Mtu anatakiwa kujifunza nayo kisha ayatendee kazi.

[1] 47:19

[2] Hilyat-ul-Awliyaa´ (07/285).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 03/02/2023