Allaah (Subhanaah) amesema:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesi upesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (07:54)

Enyi majini na watu! Hakika Mola wenu ni Allaah. Mola wenu bi maana Muumbaji wenu ambaye ndiye muabudiwa wenu Pekee anayestahiki kuabudiwa na hana mshirika:

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“… ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.”

Bi maana akapanda juu ya ´Arshi na akawa juu yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Ujuzi Wake uko kila mahali na Yeye yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe vyote. ´Arshi ndio sakafu ya viumbe na ndio kiumbe kilicho juu kabisa. Allaah yuko juu na amelingana juu yake kwa njia inayolingana na utukufu Wake. Hakuna sifa Yake yoyote inayofanana na sifa za viumbe Wake. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hakuna yeyote kabisa anayelingana Naye.” (112:04)

Allaah amesema:

يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ

“Anafunika usiku kwa mchana… “

Bi maana anafunika kimoja kwa kingine:

يَطْلُبُهُ حَثِيثًا

“… unaufuatia upesi upesi.”

Bi maana vinafuatana kwa kasi. Pindi kimoja kinaisha basi kingine kinaingia na kinyume chake mpaka Qiyaamah kisimame:

وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ

“Jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake.”

Ameumba jua, mwezi na nyota vinavyonyenyekea maamrisho Yake. Vinatii na kunyenyekea maamrisho Yake (Subhaanah):

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

“Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri.”

Yeye (Subhaanah) ndiye anayeumba na kuamrisha. Yeye ndiye Muumba ambaye maamrisho Yake ya kilimwengu ni yenye kutendeka kwa watu wote. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika amri Yake Anapotaka chochote hukiambia: ”Kuwa! – nacho huwa.” (36:82)

وَمَا أَمْرُنَا إِلَّا وَاحِدَةٌ كَلَمْحٍ بِالْبَصَرِ

”Amri Yetu haiwi isipokuwa ni moja tu – kama upepeso wa jicho.” (54:50)

Hakuna namna ya kuyakwepa maamrisho Yake ya kilimwengu. Kwa ajili hiyo amesema:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”

Neno:

تَبَارَكَ اللَّـهُ

“Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”

lina maana ya kwamba amefikia upeo wa mwisho wa baraka. Tamko hilo halimstahikii yeyote isipokuwa Allaah. Haifai kulitumia kwa mja na kusema kuwa yeye ndiye mwenye kubariki. Tamko hilo ni kama tulivyosema linatumiwa kwa Allaah pekee. Vilevile Allaah (Ta´ala) amesema:

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Amebarikika ambaye Mkononi mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni muweza.” (67:01)

Mtu anaweza kumuomba Allaah ambariki mtu fulani au kusema kuwa mtu fulani ni mwenye kubarikiwa, ama kulitumia tamko hili ni jambo lisilomstahikia Yeyote isipokuwa Allaah pekee.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 05/12/2016