147. Waislamu hawatundiki silaha kwenye mti

2 – Abu Waaqid al-Laythiyy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda Hunayn na sisi ndio punde tu tumetoka katika ukafiri. Washirikina walikuwa na mkunazi unaoitwa “Dhaat Anwaatw” wakiuadhimisha na kutundika silaha zao. Tukapita karibu na mkunazi huo tukasema: “Ee Mtume wa Allaah, tufanyie Dhaat Anwaatw kama jinsi na wao walivyokuwa na Dhaat Anwaatw. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Allaah ametakasika kutokana na mapungufu![1] Haya ndio yaleyale yaliyosemwa na watu wa Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

“Tufanyie mungu kama jinsi na wao walivyokuwa na mungu!”[2]

Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake; mtafuata desturi za waliokuwa kabla yenu.””[3]

[1] Imekuja katika upokezi mwingine:

”Allaah ni mkubwa!”

[2] 7:138

[3] Ahmad (21947), at-Tirmidhiy (2180), aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh na tamko ni lake, Ibn Hibbaan (6702) na at-Twabaraaniy (3291). Ibn-ul-Qayyim amesema kuwa ni yenye nguvu katika ”Ighaathat-ul-Lahfaan” (2/300) na akaiegemeza kwa al-Bukhaariy mahali kwengine, jambo ambalo ni kosa kutoka kwake (Rahimahu Allaah). Haiko kabisa katika ”al-Musnad as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy. Ibn Kathiyr ameitaja katika ”Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym” kupitia kwa Ibn Jariyr na Ahmad. Ni kana kwamba anaonelea kuwa at-Tirmidhiy pia ameipokea, moja katika vile vitabu mama vya Hadiyth sita.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakemea maneno yao kwa sababu ya kufanana kwake na maneno ya mayahudi, ingawa kuna tofauti ya wazi kati ya matamko na makusudio ya makundi hayo mawili. Dalili ya wazi juu ya kwamba ni dhambi kujifananisha na makafiri pasi na kujali nia ya mtu ni nzuri. Dalili ya Hadiyth hii inafanana na ile Hadiyth tuliyoitaja ambapo Maswahabah waliswali nyuma yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa wamesimama na yeye ameketi chini ambapo akawaamrisha kukaa chini.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 202-203
  • Imechapishwa: 26/11/2023