Watu wengi ambao wanakidhania vyema kila kitu na kila mtu wanaweza kufikiria kuwa watu hawa hawamaanishi yale yanayosemwa wala hata hawayafikirii pale wanapomsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) namna hiyo. Tunatamani mambo yangelikuwa hivo, lakini mtu hakifikii kila ambacho anakifirikia. Nimeyasikia mambo kutoka kwa watu ambao wanatarajiwa kuwa na elimu na wema jambo ambalo limenilazimu kuwajengea dhana mbaya na ´Aqiydah yao. Kwa mfano Shaykh mmoja, ambaye alikuwa akitoa darsa katika msikiti wa Banuu Umayyah na ambaye amekufa punde kidogo, amesema Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mkusudiwa katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye karibu – Naye juu ya kila jambo ni mjuzi.”[1]

Wakati alipokosolewa, akajaribu kulainisha kidogo kwa kutumia kitu katika tafsiri, hata hivyo bado akiendelea kung´ang´ania kuwa Aayah inamkusudia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akaambiwa asome Aayah inayofuatia:

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ

”Yeye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi.”[2]

Akaulizwa pia kama Aayah hiyo inamuhusu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akanyamaza. Yule anayejua ´Aqiydah ya wale wanaoamini Wahdat-ul-Wujuud, hashangazwi na maneno kama haya ya kikafiri kutoka kwao.

[1] 57:3

[2] 57:4

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 201-202
  • Imechapishwa: 26/11/2023