14. Kumsifu al-Albaaniy sio kuwaponda wengine

Mudiri mhariri wa gazeti la “as-Salafiyyah” kumsifia kwake al-Albaaniy sioni kama kitendo hicho ni kuwaponda wengine. Kwa sababu dalili za Kishari´ah zinaonyesha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasifia Maswahabah wake wengi pasi na kitendo hicho kuchukuliwa kuwa ni kuwaponda wengine ambao hawakusifiwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema juu ya Abu Bakr:

“Lau ningelimchagua mpenzi wangu wa hali ya juu basi ningelimchagua Abu Bakr, lakini mapenzi ya Kiislamu ndio bora. Fungeni upenyo wote katika msikiti huu isipokuwa tu upenyo wa Abu Bakr.”[1]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh):

“´Umar! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake ya kwamba hushiki njia isipokuwa shaytwaan anashika njia nyingine mbali na ile uloshika.”[2]

 Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh):

“Je, nisimuonee haya mtu ambaye anaonewa haya na Malaika?”[3]

 Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Huridhii kuwa na cheo kwangu kama cheo alichokuwa nacho Haaruun kwa Muusa, pamoja na kuwa hakuna Mtume mwingine baada yangu?”[4]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu az-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kila Mtume ana mfuasi na msaidizi maalum. Mfuasi na msaidizi wangu maalum ni az-Zubayr.”[5]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh):

“Huyu ni mjomba wangu. Wanionyeshe wengine wajomba zao.”[6]

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Abu ´Ubaydah al-Jarraah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kila Ummah una mtu mwaminifu na mtu mwaminifu wa Ummah huu ni Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah.”

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile:

“Bingwa wao juu ya mambo ya faradhi ni Zayd bin Thaabit. Bingwa wao juu ya mambo ya halali na ya haramu ni Mu´aadh bin Jabal.”

Sifa zake hizi juu ya wengine hazikuhesabika ni kuwaponda wengine. Bali alitamka kwa ujumla wao:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau mmoja wenu  atatoa dhahabu mfano wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vilivyojazwa vilivyotolewa na mmoja wao wala nusu yake.”[7]

Aidha al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) alikuwa mwanachuoni pekee Syria. Alipambana huko. Kumsifia kwa kupambana kwake dhidi ya Takfiyriyyuun na watu wa Bid´ah wengine katika nchi yake hakuzingatiwi ni kuwaponda wanachuoni wa Saudi Arabia. Kwani nao wanapambana katika nchi yao na wanastahiki fadhilah na sifa kwa yale wanayoyafanya. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِّمَّا عَمِلُوا ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ

“Wote wana daraja mbalimbali kwa yale waliyoyatenda. Na Mola wako si Mwenye kughafilika na yale waliyoyafanya.”[8]

[1] al-Bukhaariy (467) na Muslim (532).

[2] al-Bukhaariy (3294) na Muslim (2396).

[3] Muslim (2401).

[4] al-Bukhaariy (4416) na Muslim (2404).

[5] al-Bukhaariy (4113) na Muslim (2415).

[6] at-Tirmidhiy (3752). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh at-Tirmidhiy” (2951).

[7] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2541).

[8] 06:132

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fath ar-Rabbaaniy fiyd-Difaa´ ´an-ish-Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy, uk. 35-37
  • Imechapishwa: 24/11/2018