Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ama faradhi zake ni sita:

1 – Kuosha uso kukiwemo vilevile kusukutua na kupalizia. Mpaka wa uso ni pale nywele za kichwa zinapoanzia mpaka kwenye kidevu, na kuanzia kwenye sikio la kulia mpaka la kushoto.

2 – Kuosha mikono miwili mpaka kwenye visugudi.

3 – Kupangusa kichwa chote kukiwemo masikio.

4 – Kuosha miguu miwili mpaka kwenye vifundo vya miguu.

5 – Kuyafanya kwa kupangilia.

6 – Muwaalaah [kiungo kimoja kisiwahi kukauka kabla ya kuoshwa cha kufuatia].

Dalili ya hilo ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ

“Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi na panguseni vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”[1]

Dalili ya kupangilia ni Hadiyth:

 “Anza kwa Alichoanza nacho Allaah.”[2]

Na dalili ya Muwaalaah ni Hadiyth ya mtu aliyeacha sehemu bila ya kuosha. Imepokelewa kwamba wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona mtu aliyeacha sehemu katika mguu wake kiasi cha dirhamu hakikufikiwa na maji, hivyo akamuamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kurudia na kutia [wudhuu´] upya[3].

Ni wajibu kusema “Bismillaah” mtu akikumbuka hilo.

MAELEZO

Ama faradhi zake ni sita – Bi maana faradhi za wudhuu´. Hili linafuatia ile sharti ya nne miongoni mwa masharti ya kusihi kwa swalah. Faradhi za wudhuu´ ni yale mambo yake ya wajibu ambayo wudhuu´ hausihi isipokuwa kwayo.

Faradhi ya kwanza miongoni mwa faradhi za wudhuu´ ni kuosha uso. Maneno yake:

“… kukiwemo vilevile kusukutua na kupalizia.”

Ni lazima pia kusukutua na kupalizia wakati wa kuosha uso.

Kusukutua ni kule kuyachukua maji na kuyaingiza ndani ya mdomo kisha akayatema.

Kupandisha maji puani ni kule kuyachukua maji kwa kuyavuta kwa pumzi za puani kisha akayatoa.

 Imependekezwa kusukutua na kupalizia kwa kiganja kimoja akusanye kati ya mambo hayo mawili. Hivyo ndivo ilivyopokelewa katika sifa ya wudhuu´ wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Abdullaah bin Zayd bin ´Aaswim al-Aswaariy – ambaye alikuwa ni Swahabah – ambaye amesema:

“Aliambiwa: “Tutawadhie wudhuu´ wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)” ambapo akawaomba chombo, akamimika kwenye mikono yake na kuiosha mara tatu, kisha akaingiza mikono yake na kuitoa ambapo akasukutua na kupandisha maji puani kwa kiganja kimoja – alifanya hivo mara tatu -, kisha akaingiza mikono yake na kuitoa ambapo akaosha uso wake mara tatu, kisha akaingiza mikono yake na kuitoa ambapo akafuta kichwa chake na masikio, kisha akaosha miguu yake mpaka kwenye kongo mbili za miguu.”[4]

Kisha akasema:

“Namna hio ndivo ulikuwa wudhuu´ wa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Achukue maji kwa kiganja cha mkono ambapo atasukutua baadhi yake na mengine atapandisha puani, halafu atayazungushazungusha mdomoni na kuvuta kidogo puani kisha atayatoa maji puani kwa kutumia mkono wake wa kushoto.

Inapendeza kusukutua na kupalizia kwa kutumia mkono wa kulia na kutoa kwa kutumia mkono wa kushoto.

Akisukutua mara moja na akapandisha maji puani mara moja basi kumepatikana jambo la lazima. Akisukutua mara mbili na akapandisha maji puani mara mbili ndio jambo lililopendeza.  Akisukutua mara tatu na akapandisha maji puani mara tatu ndio jambo bora zaidi. Asizidishe mara tatu.

Wanachuoni wametofautiana juu ya hukumu ya kusukutua na kupandisha maji puani[5]. Maoni ya sawa ni kwamba ni mambo ya lazima. Kwa sababu mambo hayo mawili yanaingia katika kikomo cha uso. Mdomo na pua ni sehemu katika uso. Maneno yake:

“Mpaka wa uso ni pale nywele za kichwa zinapoanzia mpaka kwenye kidevu, na kuanzia kwenye sikio la kulia mpaka la kushoto.”

Hicho ndio kikomo cha uso. Mpaka wake ni pale kwenye maoteo ya nywele za kichwani mpaka kwenye kidevu, kuanzia kwenye sikio la kulia mpaka la kushoto.

Jambo la lazima wakati wa kutawadha ni kueneza maji mara moja. Kinachozingatiwa ni kule kueneza maji na sio zile mara. Akiosha mara mbili ndio bora. Akiosha mara tatu ndio bora zaidi. Asizidishe mara tatu.

Ndevu zikiwa ni ndogo na ngozi inaonekana basi ni lazima kuosha kwa ndani. Na zikiwa niyngi basi itakuwa si lazima kuosha yaliyo chini yake. Hata hivyo itapendeza kuingiza vidole ndani yake.

[1] 05:06

[2] an-Nasaa’iy (2962). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Tamaam-ul-Minnah”, uk. 88.

[3]Abu Daawuud (175) na Ahmad (15595). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (168).

[4] al-Bukhaariy (191) na Muslim (235).

[5] Maelezo ya an-Nawawiy juu ya “Swahiyh-ul-Muslim” (03/107) na “al-Majmuu´” (01/424).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 24-27
  • Imechapishwa: 13/12/2021