15. Faradhi ya pili ya wudhuu´: Kuosha mikono mwili

2 – Kuosha mikono miwili mpaka kwenye visugudi

Mtu anatakiwa kuanza na mkono wa kuume. Ataosha mikono kuanzia kwenye ncha za vidole mpaka azidi kwenye visugudi na awe kama mwenye kuanza kwenye mkono wa juu.

Baadhi ya watu wakati wanapoosha mikono wanasahau kuosha viganja vya mikono kwa hoja eti wameviosha mara tatu kabla ya kuanza kutawadha.

Ni jambo linalopendekeza kwa muislamu kuosha viganja vyake mara tatu kabla ya kaunza kutawadha[1]. Lakini mtu kuosha viganja vyake kabla ya kuanza kutawadha haina maana kwamba hatoiosha katikati ya wudhuu´. Kwa sababu kuosha viganja kabla ya kuanza kutawadha ni jambo limependekezwa na kuiosha katikati ya wudhuu´ ni faradhi. Ni lazima kuchunga wakati muislamu anapotaka kuosha mikono yake kuiosha kuanzia ncha za vidole mpaka azidi visugudi na awe kama mwenye kuanza katika mkono wa juu.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa anazidisha wakati wanapoosha mikono miwili ambapo huosha mkono wa juu mpaka akakurubia kufika makwapani. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Haazim ambaye amesema:

“Nilikuwa nyuma ya Abu Hurayrah kipindi ambapo alikuwa anatawadha kwa ajili ya swalah. Alikuwa anaosha mikono yake mpaka kufika katika makwapa. Nikasema: “Ee Abu Hurayrah! Ni wudhuu´ gani huu?” Akasema: “Ee mwanangu, Farruukh! Nyinyi mko hapa. Laiti ungelijua kwamba mko hapa basi msingetawadha wudhuu´ huo. Nimemsikia kipenzi wangu wa hali ya juu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Pambo la muumini litafika pale unapoishilia wudhuu´ wake.”[2]

Lakini maoni sahihi ni kinyume na Ijtihaad yake (Radhiya Allaahu ´anh). Kwa ajili hiyo maoni yenye nguvu katika Usuwl-ul-Fiqh ni kwamba kinachozingatiwa ni kile alichopokea na si vile alivyoona yeye[3]. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliosha mikono yake mpaka akawa kama mwenye kuanza kwenye mkono wa juu[4]. Haikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alizidisha mpaka akakurubia kufika kwenye makwapa. Haya ni maoni na Ijtihaad yake yeye. Kinachozingatiwa sio kile alichoona na kujitahidi. Isipokuwa kinachozingatiwa ni kile alichopokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (162) na Muslim (278).

[2] Muslim (250).

[3] al-Badr-um-Muniyr (06/504) ya Ibn Mulaqin.

[4] Muslim (246).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 27-29
  • Imechapishwa: 13/12/2021