16. Faradhi ya tatu ya wudhuu´: Kufuta kichwa na masikio

3 – Kupangusa kichwa chote kukiwemo masikio

Kichwa hakioshwi isipokuwa kinapanguswa. Mtu atachukua maji mapya kwa mikono yake aioshe kisha afute kichwa chake na kueneza maji. Kilichopendekezwa ni yeye kuanza na pale kwenye maoteo ya kichwa kwenda mpaka mwishoni mwake kisha arudi pale alipoanzia. Namna hiyo ndivo ilivyopokelewa kuhusu namna ya wudhuu´ wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Amr bin Yahyaa al-Maaziniy ambaye amepokea kutoka kwa baba yake ambaye amesimulia kuwa bwana mmoja alisema kumwambia ´Abdullaah bin Zayd – ambaye ni babu yake na ´Amr bin Yahyaa: “Je, unaweza kunionyesha namna ambavo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitawadha?” ´Abdullaah bin Zayd akasema:

“Ndio. Akaitisha chombo cha maji ambapo akamiminia mikononi mwake na akaiosha mara tatu, kisha akasukutua na kupalizia mara tatu, kisha akaosha uso wake mara tatu, kisha akaosha mikono yake mara mbilimbili mpaka kwenye kisugudi, halafu akafuta kichwa chake kwa mikono yake ambapo akaielekeza mwanzo hadi nwisho; akaanza mbele kwenye maoteo ya kichwa chake mpaka akaipeleka mwishoni mwake, kisha akarudi pale pahali alipoanzia, kisha akaosha miguu yake.”[1]

Kufuta kichwa hakukaririwi mara tatu. Viungo vinavyokaririwa mara tatu ni uso, mikono na miguu.

Maneno ya mtunzi:

“Kupangusa kichwa chote kukiwemo masikio.”

Asichukue maji mapya kwa ajili ya masikio. Atafuta masikio kwa yale maji aliyofutia kichwa. Baadhi ya wanachuoni wamesema kuwa atatakiwa kuchukua maji mapya, maoni ambayo ni nyonge. Maoni sahihi ni kwamba hatochukua maji mapya[2]. Kwani masikio ni yenye kufuatia kichwa.

Namna ya kufuta masikio ni kwamba atachukua vidole vya kuashiria na kuviingiza ndani ya masikio na nje ya masikio afute kwa kutumia vidole gumba.

[1] al-Bukhaariy (185) na Muslim (235).

[2] Tazama ”al-Mughniy” (01/75).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 29
  • Imechapishwa: 13/12/2021