135. Zipake rangi mvi lakini jiepushe na nyeusi

Miongoni mwa mambo yanayotilia nguvu Hadiyth hii ni kuwa Anas bin Maalik amesema:

”Siku moja wakati tulikuwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walimjia kundi la mayahudi. Aliwaona wakiwa na ndevu nyeupe ambapo akasema: ”Kwa nini hamzibadilishi?” Akaambiwa kuwa wanachukia jambo hilo. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Nyinyi zibadilisheni, lakini epukeni rangi nyeusi.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” (2/10/1). al-Haythamiy amesema:

”Katika cheni ya wapokezi yupo Ibn Lahiy´ah. Wapokezi wengine ni wenye kuaminika. Hadiyth ni nzuri.”

Kutokana na njia zingine na mapokezi mengine yanayoitia nguvu, Hadiyth ni Swahiyh kwa jumla. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu tamko hilo katika maandishi asilia:

”Tamko hili ni dalili yenye nguvu juu ya kujitofautisha nao na makatazo ya kujifananisha nao. Anapokataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kujifananisha nao kubaki mvi ambazo sio katika matendo yetu, basi kuanza kujifananisha nao kuna haki zaidi ya kukatazwa. Ndio maana kujifananisha huku kukawa ni haramu tofauti na lile la mwanzo.”

al-Munaawiy amesema:

”Hadiyth inahimiza kujitofautisha kabisa na mayahudi na manaswara, kwani kinachozingatiwa ni kuenea kwa tamko.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 191-192
  • Imechapishwa: 19/11/2023