131. Masuala yanayohusiana na jinsi ya kutangamana na mzazi kafiri

Suala la tano: Kumtendea wema mzazi ambaye ni kafiri. Amesema (Ta´ala):

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ

”Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na siku ya Mwisho kwamba wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake japo wakiwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao.” (al-Mujaadalah 58:22)

Mapenzi hayajuzu baina ya kafiri na muislamu. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ

“Yeyote atakayewafanya marafiki, basi hakika yeye ni miongoni mwao.” (al-Maaidah 05:51)

Haijalishi kitu hata kama atakuwa ni mzazi wako, kaka yako au ndugu wa karibu. Lakini kumtendea wema mzazi kafiri. Mtoto kumtendea wema mzazi wake ambaye ni kafiri kunaingia katika kulipiza wema kwa wema mwingine. Uislamu ni dini ya ikramu na wema. Unalipizwa wema kwa wema mwingine. Katika hayo kunaingia pia mtoto kumtendea wema mzazi wake ambaye ni kafiri. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا

”Tumemuusia mwanadamu juu ya wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake [akimzidishia] udhaifu juu ya udhaifu na [kumnyonyesha na] kuacha kwake ziwa katika miaka mwili ya kwamba: unishukuru Mimi na wazazi wako – Kwangu ndio marejeo ya mwisho. Lakini wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. Hata hivyo suhubiana nao kwa wema duniani.” (Luqmaan 31:14-15)

Mtoto anatakiwa kutangamana vizuri na wazazi wake makafiri kwa kuwahudumia, kuzitatua haja zao, japokuwa watakuwa ni makafiri. Kwa sababu kufanya hivi kunaingia katika kurudisha wema.

وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ

“Hata hivyo suhubiana nao kwa wema duniani na ifuate njia ya anayerudi Kwangu.”

Inapokuja katika dini anatakiwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala usifuate dini ya wazazi wako. Lakini kwa vile walikutendea wema,  wakakulea na wakakuhudumia, hivyo  basi na wewe unarudisha wema kwao hata kama watakuwa ni makafiri.

Mama yake Asmaa´ bint Abiy Bakr alikuja, akiwa ni kafiri, akamuomba amsaidie. Asmaa´ (Radhiya Allaahu ´anhaa) akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mamangu amekuja na yuko na haja. Je, nimuunge?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ndio, muunge mama yako.”

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjibu amuunge mama yake licha ya kuwa ni kafiri. Kufanya hivi hakuhusiana na mapenzi ya kidini. Hili ni kwa ajili ya kulipiza wema kwa mzazi wako aliyekulea na akakufanyia wema. Isitoshe haya ni matangamano ya kidunia. Ama matangamano ya kidini kama kuwapenda na kuwasaidia haifai. Uislamu ni dini ya ukarimu na wema. Haipingi wema japokuwa utakuwa ni wenye kutoka kwa makafiri. Unalipa wema kwa wema mwingine:

وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Hata hivyo suhubiana nao kwa wema duniani na ifuate njia ya anayerudi Kwangu halafu Kwangu ndio marejeo yenu na nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyafanya.”  (Luqmaan 31:14-15)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 166-167
  • Imechapishwa: 04/03/2019