Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili wanasema: “Sisi hatuwaombi wala hatuelekei kwao isipokuwa ni kwa sababu ya kutafuta ukurubisho na uombezi. Dalili ya ukurubisho ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Na wale wanaowafanya wengine badala Yake kuwa walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.” Hakika Allaah atahukumu baina yao katika yale yote waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye muongo, kafiri.”[1]

MAELEZO

Makafiri wa Quraysh wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakiabudu aina mbalimbali ya viumbe na waungu. Miongoni mwa vitu hivyo ni jua, mwezi, Malaika, miti, mawe na vyenginevyo. Walikuwa wakiviomba, wakiviwekea nadhiri, wakivielekea, wakikusudia viwakurubishe mbele ya Allaah na uombezi na wakisema kuwa hawakuyaomba masanamu na miti isipokuwa ni kwa ajili ya kuomba ukaribu na uombezi eti wanawakurubisha mbele ya Allaah na kuwaombea Kwake. Dalili ya hilo ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ

“Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema:]”

Bi maana badala ya Allaah:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.”[2]

Bi maana hali ya kusema kuwa hawawaabudu isipokuwa ni kwa ajili ya kutaka wawakurubishe kwa Allaah karibu.

Kisha Allaah akawahukumu katika Aayah kwa hukumu mbili:

1 – Ya kwamba ni waongo katika maneno yao na kwamba wanawakurubisha kwa Allaah. Bali ukweli wa mambo ni kwamba wanawaweka mbali Naye (Subhaanah).

2 – Amewakufurisha kwa kitendo hichi pindi wanapowaomba mawalii, wanawachinjia masanamu, miti, jua na wanawawekea nadhiri. Hii ndio shirki kubwa. Kwa ajili hiyo Allaah akawaraddi kwa kuwaambia:

إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ

“Hakika Allaah atahukumu kati yao katika yale yote waliyokhitilafiana nayo. Hakika Allaah hamwongoi aliye muongo, kafiri.”[3]

Yule mwenye kumuomba asiyekuwa Allaah, akajikurubisha, akaweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah, akamfanyia Rukuu´ asiyekuwa Allaah, basi ni kafiri kwa dalili ya Qur-aan. Haijalishi kitu hata kama ataona kuwa hawanufaishi wala hawadhuru.

[1] 39:03

[2] 39:03

[3] 39:03

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 135-136
  • Imechapishwa: 05/03/2023