Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

37 – Qur-aan ni maneno ya Allaah. Kwake ndio imeanza kwa njia ya maneno, jambo ambalo halitakiwi kufanyiwa namna, na Akaiteremsha kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya Wahy. Kwa haki kabisa waumini wamesadikisha jambo hilo na kuyakinisha kuwa ni maneno ya Allaah (Ta´ala) kikweli. Hayakuumbwa kama maneno ya viumbe. Yule mwenye kuyasikia na akadai kuwa ni maneno ya mtu basi amekufuru. Allaah amemsema vibaya, akamtia aibu na akamtishia Moto. Amesema (Ta´ala):

سَأُصْلِيهِ سَقَرَ

“Nitamwingiza kwenye [Moto wa] Saqar!”[1]

Pindi Allaah alipomtishia Moto aliyesema:

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا قَوْلُ الْبَشَرِ

“Hii si chochote isipokuwa ni maneno ya mtu!”[2]

ndipo tukajua na kuyakinisha ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Muumba wa watu na hayafanani na maneno ya watu.

MAELEZO

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ameyanukuu maneno haya yaliyopo juu ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) hali ya kuyatumia kama hoja[3]. Mshereheshaji Ibn Abiyl-´Izz (Rahimahu Allaah) amesema:

”Haya aliyosema at-Twahaawiyyah ndio haki inayofahamishwa na Qur-aan na Sunnah. Wanaona wale wenye kuyazingatia na yakashuhudiwa na maumbile yaliyosalimika ambayo hayajabadilika kwa hoja tata, shaka na maoni batili. Watu wametofautiana katika maoni tisa kuhusu maneno ya Allaah.”

Kisha akayataja na akasema:

”Maoni ya tatu yanasema kuwa maneno ya Allaah ni maana moja iliyosimama katika dhati ya Allaah; amri, makatazo, maelezo na khabari. Yakielezwa kwa kiarabu, inakuwa ni Qur-aan, na yakielezwa kwa kiebrania, inakuwa ni Tawraat. Haya ndio maoni ya Ibn Kullaab, al-Ash´ariy na wengineo.”[4]

Akasema:

”Maoni ya tatu ni kwamba maneno ya Allaah yamesimama katika dhati Yake na kwamba ameyaumba katika kitu kingine. Maoni haya ni ya Abu Mansuur al-Maaturiydiy.”[5]

Akasema:

”Maoni ya tisa yanasema kuwa Allaah (Ta´ala) daima ni Mwenye kuzungumza; Anazungumza pale anapotaka na namna Anavyotaka. Anazungumza kwa sauti inayosikika. Maneno yenyewe kama yenyewe ni ya milele ingawa sauti kwa wakati maalum sio ya milele. Haya ndio maoni ya maimamu wa Ahl-us-Sunnah.”

Halafu akasema:

”Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

Kwake ndio imeanza kwa njia ya maneno, jambo ambalo halitakiwi kufanyiwa namna… ”

Jumla hii inawaraddi Mu´tazilah na wengineo. Mu´tazilah wanadai kuwa Qur-aan haikuanza Kwake.”[6]

[1] 74:26

[2] 74:25

[3] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (12/507).

[4] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (1/173).

[5] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (1/174).

[6] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (1/174).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 24-26
  • Imechapishwa: 17/09/2024