13. Mitume ni wakweli katika yale waliyoeleza juu ya Allaah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Halafu Mitume Wake ni wakweli na ni wenye kusadikishwa, tofauti na wale wanaosema juu Yake yale wasioyajua. Na kwa ajili ya hii ndio maana amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Ametakasika Mola wako Mola Mtukufu kutokana na yote wanayoelezea na amani iwe juu ya Mitume na himidi zote ni za Mola wa walimwengu.” (37:181-182)

Hivyo kaelezea kuitakasa nafsi Yake Mwenyewe kwa waliyomuelezea wale waendao kinyume na Mitume, akawasalia Mitume Wake kuonyesha dalili ya usalama wa waliyoyasema katika mapungufu na aibu.

MAELEZO

Halafu Mitume Wake ni wakweli… – Amejieleza juu ya Nafsi Yake Mwenyewe, kama ambavyo mwandishi (Rahimahu Allaah) alivyotangulia kutaja kuhusu kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar na kwamba Yeye ni mjuzi zaidi juu ya Nafsi Yake na viumbe Wake na kwamba halinganishwi na viumbe Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kisha Mitume Wake pia ni wakweli na ni wenye kusadikishwa katika yale waliyoelezea. Yale ambayo Qur-aan inaelezea Mitume pia (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) wameyaelezea. Mbora wao, kiongozi wao na wa mwisho wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ameeleza kuwa Yeye (Subhaanah) ndiye yuko juu kabisa, amelingana juu ya ´Arshi, Yeye ndiye mwenye kutoa na kuzuia, Yeye ndiye ambaye juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Yeye ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa. Sunnah imekuja kwa sifa Zake kuu (Subhaanah) na kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Mungu wa haki anayestahiki. Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) ni wakweli katika yale waliyoelezea kuhusu Allaah.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com