13. Kazi sio udhuru wa kuchelewesha swalah

Swali 13: Wafanya kazi wengi wanachelewesha Dhuhr na ´Aswr mpaka wakati wa usiku kwa sababu eti wameshughulishwa na kazi zao au eti nguo zao ni najisi au sio safi. Kipi unachowanasihi?

Jibu: Haijuzu kwa muislamu wa kiume na wa kike kuchelewesha swalah ya faradhi nje ya wakati wake. Bali ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na wa kike ambao wanawajibika kufanya ´ibaadah kuswali swalah ndani ya wakati wake kwa kiasi cha uwezo. Kazi sio udhuru katika kuichelewesha. Vivyo hivyo najisi ya nguo na uchafu wake yote hayo sio udhuru. Ni lazima kubagua nyakati za swalah kutokamana na kazi. Ni lazima kwa mfanya kazi wakati wa swalah aoshe nguo yake kutokamana na najisi au aibadilishe kwa nguo nyingine safi. Kuhusu uchafu haumzuii mtu kuswali ndani yake ikiwa uchafu huo sio katika najisi au una harufu mbaya inayowakera wenye kuswali. Ikiwa uchafu unawaudhi waswaliji kwa dhati yake au harufu yake basi itamlazimikia muislamu kuiosha kabla ya swalah au aibadilishe kwa nguo nyingine safi ili aweze kuswali swalah pamoja na mkusanyiko.

Inafaa kwa yule ambaye amepewa udhuru unaokubalika katika Shari´ah, kama mgonjwa au msafiri, akusanye kati ya Dhuhr na ´Aswr katika wakati wa kimoja wapo na kati ya Maghrib na ´Ishaa katika wakati wa kimoja wapo. Sunnah imesihi juu ya hayo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vivyo hivyo inafaa kukusanya kwa ajili ya mvua na matopa yanayowapa uzito watu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 15/08/2022